19 March 2012

Askari wanaovujisha siri watahadharishwa

Na Grace Ndossa,
Aliyekuwa Kilimanjaro KAMANDA wa Polisi mkoani Kilimanjaro, Bw.Absalom Mwakyoma amesema baadhi ya askari wanaovujisha siri za polisi kuanzia sasa hatawavumilia na wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.


Hayo aliyasema mwishoni mwa wiki mkoani humo wakatia akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Siha kutokana na vitendo vya ujambazi na kupora mali mchana na usiku vinavyoendelea ambavyo vinadaiwa kukithiri wilayani humo. Alisema, wilaya hiyo ni mpya hivyo wananchi wanatakiwa kuwa walinzi kila sehemu iwe mchana ama usiku kwani kwa kufanya hivyo wataweza kutokomeza vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya kundi la watu ambao hawapendi maendeleo ya wengine.
Kila mmoja alipo mahali hapa anatakiwa kupokea karatasi na kuandika jina la mtu ambaye anahisi kuwa ni jambazi, anavuta bangi, wanywa gongo na wachawi ili tuweze kufanya kazi...kwani vitendo vinavyoendelea wilayani humu ni vya kutisha kutokana na majambazi kuingia mchana na kuua watu na kupora mali, alisema.

Alisema, hatua hiyo itakuwa ni siri ya kila mmoja na hakuna mtu atakayetoa siri hiyo hivyo hata baadhi ya askari ambao watabainika kuvunjisha siri za polisi kwa majambazi watachukuliwa hatua kali za kinidhamu. Hata hivyo operesheni hiyo ya kupiga kura kwa majambazi, wavuta bangi, wauza gongo na washirikiana ilifanyika katika Wilaya ya Siha eneo la Sanya Juu, na Kijiji cha Wandi Kata ya Ivaeni iliyopo wilayani humo ili kubaini
watu wote wanaofanya uhalifu katika eneo hilo. Naye Mbunge wa Jimbo la Siha ambaye pia ni Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Bw. Aggrey Mwanri alisema, wananchi wanatakiwa kuunganisha nguvu kwa pamoja na Serikali ili kuhakikisha wanakomesha uhalifu katika wilaya hiyo. "Hatua zinatakiwa kuchukuliwa ili kuweka eneo hili kuwa salama na wawekezaji waweze kuendelea kuwekeza katika maeneo yetu, kwani bila kuwepo kwa usalama wa mali na wananchi, wawekezaji watakimbia," alisema.

No comments:

Post a Comment