23 March 2012

Berko mambo safi Yanga

Na Mwandishi Wetu
KIPA namba moja wa Yanga, Mghana Yaw Berko juzi alianza rasmi mazoezi magumu, baada ya kukaa benchi tangu mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara uanze, huku akikosa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zamalek ya Misri.
Kurudi kwa Berko uwanjani kumeleta ahueni katika kikosi hicho cha Jangwani.

Berko alikuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti, baada ya kuumia katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC, uliochezwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kocha Mkuu wa Yanga Kostadin Papic alisema kipa huyo anaonekana kupona kabisa, na juzi alikuwa akifanya mazoezi magumu sambamba na wenzake hali ambayo imempa matumaini.

"Hali ya Berko inatia matumaini kwani ameanza mazoezi magumu pamoja na wenzake, hivyo naamini mchezo ujao dhidi ya Coastal Union hata akipangwa anaweza kudaka vizuri," alisema Papic.

Alisema timu yake inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi ya Kimataifa ya Tanganyika iliopo Upanga,Dar es Salaam, na wakati wowote wachezaji wake wataingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wao wa Ligi Kuu Machi 31 mwaka huu, dhidi ya Coastal Union utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani,Tanga.

Papic alisema ligi imekuwa na ushindani mkubwa sana, hivyo wanatakiwa kujiandaa kimamilifu ili waweze kushinda michezo yao yote iliyosalia, ili wajiweke nafasi nzuri ya kutetea ubingwa.






No comments:

Post a Comment