17 February 2012

Viwanja 12,000 kupimwa Ilala

Na Heri Shaaban

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilala inatarajia kupima viwanja 12,000 katika mradi endelevu wa ugawaji viwanja kwa Kata za Chanika, Msongola na Mvuti mkoani Dar es Salaam.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Meneja Mradi wa Manispaa hiyo, Bw.Jovitus Kamuzora, wakati wa kutoa taarifa ya mikakati ya manispaa hiyo, kwa Madiwani na Watendaji wa Kamati za Mazingira wa Jiji la Mwanza waliopo manispaa ya Ilala kujifunza mbinu wanazotumia kwa ajili ya kuhudumia jamii.

Bw.Kamuzora alisema kuwa wamekusudia kupima viwanja  12,000 katika mpango mkakati na nyumba ambazo zipo jirani na mradi huo hazitaguswa.

"Mara baada ya kumaliza upimaji wa viwanja 2,000 katika Kata za Kinyerezi mradi huo utahamia katika kata hizo, ambapo Chanika vitapimwa viwanja 4,000, Msongola 4,000 na Mvuti 4,000," alisema Bw.Kamuzora.

Alisema wananchi wanaoishi maeneo hayo watashirikishwa kabla mradi huo kuanza na watu waliojenga barabarani ndio watavunjiwa nyumba zao.

Mradi huo unatarajia kuanza mwaka 2012 hadi 2013 na wananchi waliokwisha jenga katika maeneo hayo, watapewa kipaumbele kabla kugawa viwanja kwa waombaji na utaratibu utakaotumika ni wa siku zote.

Kwa upande wake diwani wa viti maalum wanawake wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bi.Sarah. Nghuwani, alisema kuwa changamoto zilizopo katika Jiji la Mwanza mtu mmoja anamiliki viwanja vitano hadi kumi.

1 comment:

  1. Upimaji wa viwanja una walakini sana. Watu wengi, nikiwemo mimi tulilipie ada ya uombaji viwanja vya kinyerezi, 20,000/=. hadi leo hakuna taarifa yoyote kuhusu hatima yake. kwa hesbau za haraka si chini ya watu 20,000/ waliomba. Je fedha hizo zimeenda wapi? kwanini tusifahamishwe ni akina nani walipata viwanja hivyo?

    ReplyDelete