17 February 2012

Diwani Kisarawe ang'aka kuitwa mbumbumbu

Na Peter Mwenda, Kisarawe

MADIWANI katika halmashauri ya Kisarawe, mkoani Pwani, wameitwa mbumbumbu kwa kuidhinisha sh. milioni 500 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya elimu kwa kipindi cha mwaka 2011/2012.

Pamoja na kuidhinisha fedha hizo, madiwani hao wanadaiwa kutenga fedha nyingi zaidi ya hizo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa halmashauri na manunuzi ya gari.

Madai hayo yalijitokeza juzi katika warsha ya utawala bora iliyofanyika mjini ambayo iliandaliwa na Asasi ya Mfuko wa Maendeleo Kisarawe (KIDEFO), ikihusisha wakazi wa Kata ya Msimbu, Msanga, asasi za kiraia na makundi maalumu.

Akitoa mada katika warsha hiyo, Mwezeshaji kutoka DEFCO, Bw. Bugi Ngeseni, aliwaambia washiriki hao kuwa madiwani hao wameidhinisha sh. milioni. 500 ambazo hazitoshi kuendeleza sekta hiyo hasa kwa kuzingatia uduni wa elimu inayotolewa wilayani humo.

“Fedha zilizotengwa katika sekta ya elimu ni chache sana wakati zile zilizoidhinishwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi na manunuzi ya gari ni kubwa, ujenzi wa nyumba imetengwa milioni 180, ununuzi wa gari milioni 120, na lingine la ukaguzi milioni 140.


“Mimi nimesoma Sekondari ya Mwaneromango, ambayo imesomesha viongozi wengi na wataalamu katika sekta mbalimbali akiwemo mbunge wa Kisarawe, Bw. Suleiman Jafo, shule hii imeshika nafasi ya pili kutoka mwisho katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2011,” alisema Bw. Ngeseni.

Aliongeza kuwa, Wakurugenzi wamekuwa wakiunda kikundi cha madiwani wao ambao wanawaburuza katika vikao vya halmashauri kwa sababu ya elimu zao ni darasa la saba.

Bw. Ngeseni alisema elimu hiyo haiwawezeshi kuwa na uwezo wa kujenga hoja katika vikao vya halmashauri ambavyo taarifa zake zinaandikwa kwa lugha ya kiingereza.

Mshiriki wa warsha hiyo, Bi. Monica Mahoza, alisema tatizo la elimu kwa madiwani wa Kisarawe ni kubwa hivyo ni vigumu kuchanganua bajeti ya halmashauri.

Kauli ya madiwani hao kuitwa mbumbumbu, ilimfanya Diwani wa Vikumburu Bw. Juma Dihonga kwa tiketi ya CUF, kucharuka na kupinga hatua ya mtoa mada kuwaita mbumbumbu.

Hata hivyo, Bw. Dihonga alilazimika kutulia baada ya washiriki kuungana na watoa mada wakisisitiza kuwa, madiwani hao hawakutumia busara ya kutenga fedha chache kwa maendeleo ya elimu na kutenga fedha nyingi kwa mambo yasiyo ya msingi.

“Nimekubali maoni ya wananchi wa Kisarawe, naahidi sitakuwa tayari kupitisha bajeti ambayo haina manufaa kwa wananchi,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Jinsia wilayani humo, Bi. Gretude Mwanakadudu, alisema amewahi kusikia wenyeji wa Kisarawe walikataa ujenzi wa hospitali ambayo hivi sasa imejengwa mkoani Kilimanjaro ya KCMC, kutokana na msimamo wa udini.



No comments:

Post a Comment