Na Anneth Kagenda
KANISA la Ufufuo na Uzima lililopo chini ya Mchungaji Kiongozi Bw. Josephat Gwajima, jana lilizizima baada ya viongozi wa Chama na Serikali wakiwamo Mawaziri kufika kwenye Ibada maalum ya Uzinduzi wa Mpango wa Program ya 'Neno la Hekima kutoka kwa Kiongozi'.
Kadharika, ibada hiyo pia ilihusu kutoa shukrani kwa Mungu juu ya uponyaji wa Naibu Waziri wa Ujenzi Dkt. Halson Mwakyembe ambaye pia alizuru kanisani hapo kwa ajili ya kutoa shukrani.
Akizungumza wakati wa ibada hiyo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kati Bw. Samweli Sitta, alisema, "kwanza ninamshukuru Mungu kwa kumponya Dkt. Mwakyembe na wale wote waliohusika katika hili watakiri na kuamini kwamba Mungu siyo wa mchezo, na mimi ninakiri adharani kwamba alipewa sumu na Mungu kamponya sasa hao waliohusika wajue kwamba hawawezi kupambana na nguvu ya Mungu kwani mkono wake ni mrefu kuliko kitu chochote," alisema,
"Kama Dkt. Mwakyembe hakupewa sumu basi vyombo vinavyo endelea na uchunguzi vitwambie ilikuaje mpaka akafikia hali hiyo, kuna watu wanapenda madaraka makubwa na kusahau Taifa letu na watanzania kwa ujumla lakini hawa waliokuwa wanamchezea waziri sasa imekula kwao," alisema Bw. Sitta.
Alisema, kupewa sumu kwa Dkt. Mwakyembe ni kutokana na watu wenye uroho wa madaraka waliotaka kummaliza kabisa na kusema kuwa kama Mungu hajapanga katu yale yanayopangwa na binadamu hayawezi kutimia, na kwamba pamoja na kubadilika ngozi hadi kufikia ngozi ya nne aliyonayo hivi sasa wabaya hao walidhani atakufa lakini hilo halikuwezekana kutokana na maombi ya madhehebu mbalimbali.
"Nilienda mpaka hospitali aliyolazwa, nilishindwa kuamini kile nilichokuwa nakiona, Dkt. ngozi yake ilikuwa kama ya tembo wakati miguu utadhani kaugua matende na pale mfanyakazi wa hospitali anapofagia ni kama anafagia unga na pia tuliambiwa kwamba sumu aliyokula haikuingia kwenye moyo, figo wala maini bali ilitoka nje ndio maana madhara haya yakajitokeza alafu leo mtu anasema hakunywa sumu," alihoji
"Kutokana na haya yote yanayoendelea kutokea tutaendelea kuomba siku itakuja wala rushwa watajulikana ndani ya nchi hii na machozi ya watanzania hayawezi kukauka hivi hivi na tutarudi kwenye mstari ulionyooka siyo tu mtu anampita mwenzake juu na kuondoka zake" alisema
Alisema nchi hii imekuwa na tatizo sugu la kukumwa na ibirisi wa rushwa jambo linalosababisha kutotendeka kwa haki na kama inatendeka basi imepinda kwani hata ukitakiwa kupata fidia basi utapewa nusu huku wanafunzi wakipiga kelele juu ya mikopo yao lakini benki zinachelea kutoa fedha hiyo.
Hata hivyo alisema, kuna viongozi ambao wanatakiwa kuombewa zaidi kwa Mungu kutokana na kwamba wamekuwa wakiasi na pia wamekuwa wakitumia uongozi wao kuliibia Taifa huku wakiwaacha watanzania wakiangaika wasijue cha kufanya.
Naye Mchungaji Gwajima, alisema lengo mahususi la kuzindua program hiyo ni kutokana na kuwapo changamoto nyingi hasa zile za kisiasa, kiuchumi na kijamii tangu kupata Uhuru wake mwaka 1961.
"Serikali inayoshika hatamu imetoa uhuru wa kuabudu licha ya Taifa kuwa na madhehebu mengi na makabila mengi, hili ni jambo jema zuri na la kujivunjia hivyo kama kanisa tunamshukuru Mungu kwa hilo, hivyo basi ni dhahiri kabisa serikali haiwezi kufanya kazi pekee bila kushirikiana na Taaisi za kidini katika kuleta maendeleo kwa watu wake," alisema Mchungaji Gwajima.
Malengo mengine ni kanisa kutambua nafasi yake na kuombea Taifa na viongozi wake kuanzia Rais, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, watendaji wa Kata na Mitaa na chama ili waongoze katika hekima na busara kutoka kwa Mungu pamoja na kuombea nchi ili kuendelea kuwa kitovu cha Amani kwa watanzania wenyewe na nchi za jirani.
Naye Dkt. Mwakyembe, alitoa shukrani kwa kusema kuwa ni ukweli usiopingika kwamba Mungu kamponya na kuutaka umati uliokuwepo kanisani hapo kuendelea kumwombea pia Mwandosya aliyeko India.
"Nashukuru kwa mema na baraka bila kuchoka kwani tangu Oktoba 9, nilivyoondoka hapa na kufika hospitalini Oktoba 10, leo ndio ninavaa viatu hivyo lazima nitumie mda wangu mwingi kuzunguka makanisani kumshukuru Mungu na kumzomea shetani," alisema Dkt. Mwakyembe.
Viongozi wengine waliokuwepo kwenye ibada hiyo ni pamoja na Mbunge wa Same Mashariki Bi. Anne Kilango, Mbunge Viti maalum Mbeya Bi. Ilda Mgoe, Mbunge wa Mbeya Bw. James Lembeli, aliyekuwa Mbunge wa Vunjo Bw. Aloyce Kimaro.
Kwa upande wake Bw. Lembeli, alimtaka Mchungaji Gwajima kuhakikisha hakuna kiongozi mchawi wala mla rushwa anaingia kanisani hapo lakini pia nikusihi uliombee bunge letu kwani watenda dhambi wake wengi pamoja na wala rushwa hivyo kwa pamoja tuombe Amani na Utukufu.
"Na vita tuliyonayo kuu ni wizi, ufisadi na rushwa na hivi ndivyo vilivyokidhiri hivyo kwa pamoja watanzania tumwombe Mungu atunusuru na majanga haya ikiwa ni pamoja na kutokubali watu wa aina hii kuingia katika kanisa hili ambao badaye wanaweza kuambukiza mbegu mbaya," alisema Bw. Lembeli.
.
No comments:
Post a Comment