01 February 2012

SHIRIKISHO la mpira wa miguu nchini (TFF)

Na Amina Athumani

SHIRIKISHO la mpira wa miguu nchini (TFF) limesema linatafuta uwezekano wa timu ya soka la wanawake Twiga Stars kucheza mechi za kirafiki na timu za Uganda na Kenya kabla ya kukutana katika mchezo wao wa kuwania kufuzu Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya Ethiopia unaotarajiwa kuchezwa mwezi Mei mwaka huu.

Akizungumza Dar es Salaam juzi katika mahojiano yaliyorushwa moja kwa moja katika Televisheni ya ITV katika uwanja wa Taifa muda mchache baada ya mechi kati ya Twiga Stars  dhidi ya Namibia kumalizika, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema wamefurahishwa na ushindi mkubwa wa timu hiyo walioupata nyumbani na kwamba watahakikisha timu hiyo inapata maandalizi ya kutosha ili iweze kufanya vema katika mchezo wao  dhidi ya Ethiopia.

"Tutaangalia uwezekano wa kuitafutia timu hii mechi za kirafiki kwa timu za Uganda na Kenya kabla ya kukutana na mshindi kati ya Ethiopia na Misri,"alisema Osiah.

Naye kocha wa timu ya Twiga Stars Boniface Mkwasa alisema Dar es Salaam jana kuwa kwa sasa timu hiyo wameipa mapunziko mara baada ya kuibuka na ushindi huo mkubwa wa magoli 5-2 na kufanya kuibuka na ushindi mkubwa wa idadi ya magoli 7-2  baada ya kupata magoli 2-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Namibia.

"Kibali cha kuanza mazoezi kinatolewa na TFF hivyo bado sijajua wachezaji wangu watapunzika hadi lini ila kibali kitakapotolewa basi tutaanza mazoezi,"alisema Mkwasa.

Twiga Stars ambayo inasaka nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Afrika kwa wanawake itakutana na Ethiopia ambapo ikishinda mchezo huo nyumbani na ugenini itakuwa imekata tiketi ya kushiriki fainali hizo.


No comments:

Post a Comment