17 February 2012

Ufisadi Maliasili

*Kamati ya Bunge yabaini matumizi holela ya fedha
*Wizara yakiri kutofahamu idadi watalii waingiao nchini
*Wapata hati chafu miaka mitatu mfululizo kuanzia 2008

Salim Nyomolelo na Rachel Balama

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imebaini ufisadi wa matumizi mabaya ya fedha katika Wizara ya Maliasili na Utalii kabla hazijaingizwa kwenye vitabu vya Serikali.

Ufisadi huo ulibainika Dar es Salaam jana kwenye kikao ambacho  kilishirikisha wajumbe wa kamati hiyo na watendaji wa Wizara.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa kamati hiyo Bw. John Cheyo, alisema ripoti ya Mkaguzi wa hesabu katika Wizara hiyo imeonesha kuwa, watendaji wana utaratibu wa kutumia fedha za umma kabla hazijaenda hazina jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Watendaji wa Wizara hii wana utaratibu mbovu wa kukusanya mapato na kuwasilisha baadhi ya fedha hazina, nyingine mnatumia kwa matumizi gani,” alihoji Bw. Cheyo.

Aliongeza kuwa, kutokana na utendaji mbovu, Wizara hiyo imekuwa ikipata hati chafu miaka mitatu mfululizo tangu mwaka 2008 jambo ambalo ni aibu kwa Wizara husika.

“Sisi kama kamati, hatuliziki na hesabu zako kwa kuwa tangu mwaka 2008 hadi sasa, mmekuwa mkipata hati chafu na inazidi kuwa chafu zaidi,” alisema Bw. Cheyo.

Akifafanua zaidi, Bw. Cheyo alisema taarifa hizo za hesabu zinaonesha kuwa, mapato ya Wizara hiyo yanashuka kila mwaka.

“Mwaka 2009 makusanyo yalikuwa sh. trilioni 1.7 na serikalini zilipelekwa sh. bilioni 77, mwaka 2010 walikusanya mapato ya sh. trilioni 1.2, serikalini walipeleka sh. bilioni 52.

Alisema kutokana na kushuka kwa mapato kila mwaka na ukosefu wa tawkimu sahihi, ndiyo sababu inayoifanya Wizara hiyo ishutumiwe kupeleka twiga nje ya nchi kwa kuwa hakuna vielelezo.

“Hesabu zinaonesha mwaka 2010, fedha za miradi zilikuwa sh. bilioni 26, mwaka 2011 zimeshuka hadi sh. bilioni 10,mwaka huu inaonesha bajeti ni ziro, ina maana hakuna miradi inayoendelea katika Wizara hii mwaka huu,” alisema.

Kamati hiyo iliitaka Wizara kuwatoza watalii fedha za Tanzania wanapofanya malipo ya kutembelea maeneo yenye vivutio badala ya kutoza kwa dola za Marekani.

Akijibu tuhuma hizo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi. Maimuna Tarish, alisema jitihada za kurekebisha makosa yanayochangia wapate hati chafu zinaendelea kufanyika ambapo ifikapo Januari 2013, utaratibu wa kupata hati safi utakuwa umekamilika.

Katika hatua nyingine Bi. Tarish, alipoulizwa kama ana taarifa za kutokuwepo kwa daftari la kujua idadi ya watalii wanaoingia na kutoka nchini , alisema hiyo ni changamoto kubwa kwa wizara.

“Ni kweli Wizara haina mfumo wa pamoja wa daftari ili kujua idadi ya watalii wanaokuja nchini kutembelea vivutio mbalimbali lakini katika idara zote zilizopo chini yetu, kuna madaftari ya takwimu.

“Nakiri kwamba hii ni chanhamoto kubwa, kama Wizara tunaipokea na tutaifanyia kazi kuhakikisha idara zote zilizopo chini yetu zinaunganishwa, kuwa na daftari moja na kuliweka katika mfumo wa kieletroniki ili kujua idadi ya watalii wanaoingia na kutoka,” alisema Bi. Tarish.

Katika hatua nyingine, Bi. Tarish mapato mengi ya Wizara hiyo yanapotea kwa saababu Serikali haina ndege yake kwani nyingi zinamilikiwa na mashirika mbalimbali jambo ambalo linachangia mapato ya Wizara kushuka.

“Serikali iliangalie hili kwa mapana yake angalau tuwe na ndege ili fedha za malipo, zibaki nchini na kama hatutafanya hivyo, fedha zote za nauli zitakwenda kwenye mashirika ya nje,” alisema.

Hata hivyo, kamati hiyo ilimuagiza Mhasibu wa Wizara kukaa na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ili kurekebisha kasoro zilizopo na kuhakikisha matumizi ya fedha zote yanakuwepo katika vitabu vya Serikali.

2 comments:

  1. haya tumeyazoa hiyo ndio Tanzania yetu.

    ReplyDelete
  2. NAOMBA WABUNGE WAPIGE KAMBI MALIASILI KAMA WALIVYOTAKA KUFANYA KIVUKO CHA KIGAMBONI ILI KUINGIA KWA UNDANI MAHESABU YA WIZARA HII.

    MHASIBU WA WIZARA HII NA HATA MKAKUZI WA MAHESABU YA SERIKALI WAKO KWENYE MKUMBO MMOJA WA HUJUMA.

    KUANZIA HUKO NYUMA, HII WIZARA INA VITABU VIWILI VYA KUPOKEA MAPATO. WENYE VITALU VYA UWINDAJI WANAIANGAMIZA NCHI KIMAPATO.

    KAMA KAWAIDA MSIULIZE USHAHIDI. FANYENI UCHUNGUZI WA KITAALAM. lINGANISHENI RIPOTI ZA WANYAMA WALIOULIWA KUTOKA KWA GAME OFFICER NA ILE YA WAHASIBU NA MTAONA VITUKO.

    kUMBUKENI LILE SAKATA LA NORWAY! COVER UP TUPU.

    ReplyDelete