Na Anneth Kagenda
WAZIRI wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Dkt. Emmanuel Nchimbi, amemaliza tofauti kati ya Mbunge wa Arusha Mjini Joseph Mbilinyi a.k.a Sugu na Mkurugenzi wa Clouds Media Rugemalila Mutahaba.
Upatanisho huo ulifanyika jana kwenye kikao cha mwisho kati ya Dkt. Nchimbi, Sugu, Bw. Mutahaba na Mbunge wa Singida Mashariki Bw. Tundu Lisu.
Katika taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari jana, katika upatanishi huo pande zote mbili ziliridhika kuwa msingi wa mgogoro wao ni kila upande kuwa na kundi la wasanii na kuamini kuwa upande mmoja hautendei haki upande mwingine.
"Pande hizo mbili ziliridhika pia mgogoro huo baina yao badala ya kuimarisha mchakato wa kuhamasisha upatikanaji wa Haki za wasanii, unadhoofisha jitihada hizo," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema kuwa pande hizo ziliridhika pia kuwa mgogoro baina yao unajenga uhasama na utengano mkubwa miongoni mwa wasanii, ambao wanapaswa kuungana kudai na kusimamia maslahi yao hivyo Sugu na Ruge wamekubaliana yafuatayo.
Wanamaliza mgogoro na uhasama baina yao kuanzia jana, wanashirikiana kufanikisha haki na jitihada ya kuinua maslahi ya wasanii na pia kufanya jitihada ya pamoja ya kuunganisha Vyama vya Wasanii vya TUMA na TFU, ili kutetea maslahi ya wasanii wakiwa na Umoja zaidi.
Makubaliano mengine ni kwamba wanawaomba watu wote wanaowaunga mkono wamalize uhasama na kufungua ukurasa mpya na ushirikiano baina yao.
No comments:
Post a Comment