Na Amina Athumani
TIMU za taifa za ngumi, riadha na judo zitakazofuzu kucheza michezo ya Olimpiki itakayofanyika Uingereza, Julai mwaka huu zitapiga kambi ya mwezi mmoja jijini London, kabla ya michezo hiyo kuanza.
Kambi hiyo ambayo itaratibiwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), itafanyika mwezi mmoja kabla ya mashindano hayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, kwa upande wa kambi ya timu ya ngumi inayojiandaa kufuzu kucheza Olimpiki katika mashindano yatakayofanyika Casablanka, Morocco Katibu Mkuu wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Makore Mashaga alisema mabondia wataingia kambini rasmi Machi Mosi mwaka huu.
Alisema wakati wanajipanga kwenda Casablanka, mabondia wote 17 wa timu ya taifa wataanza kambi ya kwenda na kurudi nyumbani wakati BFT ikiendelea kufanya utaratibu wa kuwatafutia ufadhili wa hoteli.
Mashaga alisema wachezaji hao watafanya mazoezi katika Uwanja wa ndani wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya kujiandaa na mashindano ya kufuzu Olimpiki ambayo yanatarajia kufanyika Aprili mjini Casablanka.
"Mei mwaka huu timu zilizofuzu zitaweka kambi Uingereza kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki, lakini sisi ili kujiimarisha zaidi na ili tuweze kufuzu Olimpiki, wachezaji wote wataanza kambi rasmi Machi Mosi katika Uwanja wa ndani Taifa Dar es Salaam," alisema Mashaga.
Katibu huyo alisema hadi jana mchana, walikuwa wanaendelea na kikao cha kumchagua kocha atakayeifunza timu ya taifa ya mchezo huo ambayo awali ilikuwa chini ya kocha raia wa Cuba, Hurtado Primentel.
No comments:
Post a Comment