Na Florah Temba, Kilimanjaro
MADEREVA wa magari madogo maarufu kama Hiace (daladala) yanayofanya safari za kutoka Moshi kwenda Marangu, Mwika, Rombo na Holili mkoani Kilimanjaro wamegoma kwa zaidi ya saa sita wakilalamikia Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuwaomba rushwa.
Wakizungumza katika Stendi Kuu ya Mabasi Mjini Moshi jana, madereva hao walisema wamekuwa wakipata usumbufu barabarani kila siku hali ambayo imewafanya kushindwa kusonga mbele kimaendeleo kutokana na kwamba fedha ambazo wamekuwa wakifanyia kazi nyingi zimekuwa zikiishia polisi.
Walisema, Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (Trafic) hapo awali, walikuwa wakiwasimamisha kila kituo na kuwaomba sh.2,000 ambapo waligoma na kwenda kutoa taarifa katika Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).
Walisema, baada ya kutoa taarifa hizo TAKUKURU, askari hao waliogopa kuchukua tena fedha barabarani wakihofia kupewa fedha za moto na badala yake kwa sasa wameanza kuwakamata na kuwabambikizia makosa na kutakiwa kutoa sh. 30,000 kwa kila kosa.
“Kwa kweli tumechoka kunyanyaswa na trafiki barabarani, kwani wamekuwa wakitukamata kila kituo na kila tunapokamatwa tunatakiwa tutoe sh.30,000 na kama hatuna tunaambiwa tutoe sh.10,000 ili watuachie;
"Huu ni uonevu, kwani hadi sasa tumeshindwa kuendesha familia zetu kutokana na kujikuta fedha tunazofanyia kazi zikiishia barabarani, kwani hapa fedha zinatakiwa nipate, mmiliki alipwe dereva na hata kondakta ”alisema, Bw. Editon Kimaro miongoni mwa maderava ambaye basi lake linafanya safari kati ya Moshi na Holili.
Naye, Bw.Raphael Mfutakamba mdau wa usafirishaji na uchukuzi mkoani Kilimanjaro alisema, polisi wa usalama barabarani wamekuwa kikwazo kikubwa barabarani kutokana na kwamba kumekuwa na vituo vingi, barabarani na kikubwa wamekuwa hawakagui makosa na badala yake wamekuwa wakiomba rushwa.
Akitolea mfano wa kutoka Moshi hadi Himo, Bw.Mfutakamba alisema eneo hilo ambalo lina kama kilomita 20 lina vituo vya askari barabarani zaidi ya sita na katika vituo vyote gari inasimamishwa na wakati mwingi huwa wanasimamishwa na kukamatwa bila sababu yoyote ya msingi.
Alisema, tatizo kubwa analoliona ni viongozi kukaa eneo moja kufanya kazi kwa muda mrefu hivyo kushindwa kuwajibika ipasavyo na hivyo kuiomba Serikali kuingilia na kuangalia kwa karibu malalamiko ya madereva na wamiliki wa magari mkoani humo kutokana na kwamba wamekuwa wakilalamika mara kwa mara pasipo kuchukuliwa hatua zozote.
Alisema, kuna haja ya kutolewa elimu ya usafirishaji kwa wamiliki na kwa madereva ili kuweza kumaliza matatizo kama hayo ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kutokana na kwamba polisi wamekuwa wakikamata tu magari pasipo kutoa elimu wala kumuelimisha dereva ili aweze kujirekebisha.
Akizungumzia tatizo hilo la mgomo Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw.Leonidas Gama alikiri kuwepo kwa mgomo huo na kusema kuwa tayari amemtuma Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Bi.Bernadeta Kinabo ili kwenda kuzungumza na madereva na kusitisha mgomo.
Aidha akizungumzia malalamiko ya rushwa yanayotolewa dhidi ya askari wa kikosi hicho, Bw.Gama alisema ili kuweza kumaliza tatizo hilo madereva wanapaswa kugoma kutoa fedha kwao na badala yake wanapotakiwa kutoa fedha watoe taarifa kwa uongozi husika ili waweze kuchukuliwa hatua.
“Suala hili la rushwa kwa matrafic kimsingi siwezi kulitolea ukweli, na badala yake nawaomba madereva wakatae kutoa rushwa kwao na pindi wanapokamatwa na kutakiwa watoe fedha watoe taarifa kwa uongozi husika ili waweze kuchukuliwa hatua katika hili, tunahitaji ushirikiano kwani tusiposhirikiana kulidhibiti hili tunazidi kulikuza tatizo na kulifanya kuwa sugu," alisema Bw.Gama.
No comments:
Post a Comment