07 February 2012

Simba yawaomba radhi mashabiki wake

Boban, Nyoso wapewa unahodha
Na Elizabeth Mayemba
UONGOZI wa Klabu ya Simba na wachezaji wake wameomba radhi wanachama na mashabiki wa timu hiyo, kutokana na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Villa Squad, katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo, Ibrahim Masoud 'Maestro' alisema kutokana na kipigo hicho wameona wawaombe radhi wanachama na mashabiki wao, kwani wanajua kwa kiasi kikubwa matokeo yale yaliwaudhi na kuwakosesha raha.

"Japokuwa mpira una mambo matatu, kufungwa, kushinda na sare, lakini kwa jinsi Villa walivyo hatukutarajia kupoteza pointi, kwani timu yetu ina maandalizi mazuri tofauti na wapinzani wetu, hivyo tumeona tuchukue fursa hii kuwaomba radhi wanachama wetu na mashabiki," alisema Maestro.

Alisema huu ni utaratibu ambao wamejipangia kuanzia sasa, wa kuomba radhi pale watakapokuwa wakivurunda katika michezo mbalimbali, hivyo wanaimani kabisa mashabiki wao watawaelewa kwa hilo.

Pia Maestro alisema, uongozi wa klabu hiyo kuanzia mechi ijayo dhidi ya Azam FC, wataanza kuwachunguza wachezaji wao ambao watakuwa wanacheza chini ya kiwango na nidhamu kwa ujumla na watachukua hatua kali za kinidhamu kwa yeyote atakayebaika kufanya hivyo.

Mwenyekiti huyo alisema wakiwa kama viongozi walikaa na wachezaji na kuwataka kuwasilisha maoni yao kwa uongozi pale wanapoona inabidi, ili timu yao iweze kufanya vizuri katika mechi zake za Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.

Katika hatua nyingine, kiungo wa timu hiyo, Shomari Kombe amekuwa mchezaji bora wa mwezi katika mechi za Ligi Kuu zinazoendelea nchini na hivyo kupewa tuzo na viongozi wake na kuongezewa sh. 200,000 katika mshahara wake wa mwezi uliopita.

Kapombe amepewa tuzo hiyo baada ya kuonesha kiwango kikubwa uwanjani na nidhamu ndani na nje ya uwanja.

Wakati huohuo, uongozi wa klabu hiyo umemteua kiungo wake Haruna Moshi 'Boban' kuwa nahodha msaidizi akiwa na beki Juma Nyosso wakimsaidia Kaseja ambaye ndiye nahodha wa timu hiyo.

Maestro alisema uongozi wa klabu hiyo umeona kuna kila sababu ya kuwa na manahodha watatu, kwani mara nyingi wakati wa mechi Boban amekuwa akiwasemesha wachezaji wenzake pale anapoona wamepotea, hivyo wameona ni vyema wakimwongeza kuwa nahodha msaidizi.

"Mchawi mpe amlee mwanao, kwani mengi yanazungumzwa kuhusu Boban kwamba hana nidhamu ndani na nje ya uwanja, sasa sisi kwa kutambua umuhimu wake tumempa nafasi hiyo, kama atakubali kuiua timu yake haya," alisema.


2 comments:

  1. Uongozi wa Simba wasifikirie tuu kuwaomba radhi mashabiki wangaalie ni jinsi gani mashabiki wanaweza wakawa wadau katika kuendesha timu. Club ya Simba itabidi iendeshwe kwa mfumo tofauti na wa sasa ili kila mtu awe na hisa na sio mapenzi katika kilabu.

    ReplyDelete
  2. We Maestro timu yako simba mmechemsha, hamna lolote. Huwezi kusema hukutarajia kupoteza pointi, mchezo ni mchezo tuu, leo imekula kwako kubali matokeo.
    Badala ya kuwaomba washabiki radhi tizama ni wapi kulikuwa na hitlafu kusababisha kufungwa.........

    ReplyDelete