07 February 2012

Yanga yahofia kwenda Misri

Yaomba mechi ichezwe moja
Na Zahoro Mlanzi
KLABU ya Yanga imeliandikia barua Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuomba mechi yao dhidi ya Zamalek ya Misri ichezwe katika mkondo mmoja Dar es Salam pekee kwa ajili ya kuhofia usalama wa wachezaji na mashabiki wao.
Yanga inatarajiwa kuumana na miamba hiyo ya Misri katika mechi ya awali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Februari 18, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na marudiano kufanyika wiki mbili baadaye jijini Cairo.

Lakini kutokana na hali ya usalama kwa hivi sasa nchini Misri kuwa si shwari baada ya vurugu kubwa zilizotokea katika mechi ya Ligi Kuu ya nchi hiyo, kati ya Al Ahly na Al Masri kwenye Uwanja wa Port Said na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 74 na majeruhi zaidi ya 1,600, ndiyo maana Yanga imeomba hivyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Celestine Mwesigwa alisema wameiandikia CAF barua kupitia TFF (Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania) wakiomba mechi hiyo ichezwe moja tu, Dar es Salaam.

"Tumelipokea kwa masikitiko makubwa tukio lililowatokea wenzetu huko Misri, kama ilivyotangazwa kwamba watu wengi wamepoteza maisha na wengine kujeruhiwa, hivyo tunalazimika na sisi kuchukua hatua za kiusalama, ili yasije kutokea kama hayo," alisema.

"Tuna mechi ya marudiano na Zamalek baada ya hii tutakayocheza Februari 18 hapa nyumbani, hivyo kutokana na sababu za kiusalama tumeona ni vizuri tukaiandikia CAF barua na kuiomba mchezo wetu sisi na Zamalek, uwe ni mmoja tu kutokana na hali hiyo ya vurugu," alisema.

Alisema kwa mujibu wa kanuni za CAF, kuna vipengele vinatoa fursa hiyo na ndiyo maana wakavifuata na kilichobaki kwa sasa wanasubiri majibu kutoka CAF, kujua kama itawezekana katika hilo au watawaeleza nini juu ya mechi yao ya marudiano.

Katibu huyo alisema katika barua hiyo waliyoipeleka Ijumaa TFF, wamependekeza mechi hiyo moja ichezwe Dar es Salaam tu kama kanuni zinavyoeleza kwamba kati ya nchi mbili, moja ikiwa na vurugu kama hizo, basi mechi hiyo ipigwe katika nchi iliyobaki.

Wakati huohuo, Mwesiga alisema kwa mujibu wa Ubalozi wa Misri nchini, Zamalek inatarajiwa kutua Dar es Salaam alfajiri ya Februari 17 na jioni ya siku hiyo itafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Taifa na itaondoka Jumatatu.

Awali kutokana na tukio hilo, Serikali ya Misri kupitia Waziri Mkuu wake, Kamal Al-Ganzouri iliwatimua viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kwa madai ya kuzembea na kusababisha vifo vya watu hao.

Mbali na hilo, pia iliagiza uchunguzi wa kina ufanyike ikiwa ni muda mfupi baada ya uongozi wa chama hicho, kusimamisha ligi hiyo kwa muda usiofahamika.

2 comments:

  1. Panga mechi sehemu nyingine. Hao waarabu sikuzote twawajua kuwa hawana ustaarabu.

    ReplyDelete
  2. nendeni tu sababu mshaharibu,ili mkawafunge kwao mrudi naushindi mungu atawasaidia na sisi tunawaombea.

    ReplyDelete