07 February 2012

Bongo Movie FC yainyoosha Kadansi FC

Na Victor Mkumbo
TIMU ya soka ya wasanii wa filamu nchini (Bongo Movie FC), juzi iliibuka na ushindi wa mabao 4-3 katika mchezo wa hisani dhidi ya wasanii wa bendi (Kadansi FC) uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo ulikuwa wa hisani kwa ajili ya kuwachangia waathirika wa mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa mwaka jana katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Katika mchezo huo ulioandaliwa na kituo cha redio Times kwa kushirikiana na Compact Media timu hizo zilionesha kandanda safi lililokuwa kivutio kwa mashabiki wa soka waliofika uwanjani hapo.

Timu hizo hadi zinakwenda mapumziko zilikuwa sare ya 2-2, ambapo mabao ya Kadansi FC yalifungwa na Ben Bevianga na Josee Mara, wakati ya Bongo Movie yalipachikwa wavuni na Capturado Nyani na Ambani Mtitu.

Kipindi cha pili Bongo Movie, walicharuka na kufanya mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na kufanikiwa kuongeza mabao mengine yaliyofungwa na Messin Hassan na Idrisa Makupa 'Kupa', wakati bao la tatu la Kadansi FC lilifungwa na Heri Edward.

Mgeni rasmi katika mchezo huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mecky Sadick, ambaye aliwashukuru wasanii hao na kusema kuwa ni mfano wa kuigwa.

Hata hivyo alisema wasanii wanatakiwa kuwa na umoja kwa kucheza mechi mbalimbali kwa ajili ya kujenga afya zao na si kusubiri mpaka majanga yanapotokea.

Alisema pia wanaweka uiano mzuri kati yao na mashabiki na wapenzi wa kazi zao, kuliko kuwaona katika televisheni na hivyo kuwaona moja kwa moja kupitia michezo na kuweza kuwa nao karibu.

“Juhudi walizozionesha wasanii hawa ni mfano wa kuigwa kutokana kuonesha kitu kinachoonesha kuwajali mashabiki wao, hivyo tunawapongeza na wawe na moyo huo huo kwa kutoa misaada katika mambo mbalimbali,” alisema.






















No comments:

Post a Comment