Na Mwandishi Wetu,
Morogoro
UBORA wa miundombinu katika Mto Kilombero imeelezwa kuwa ni suala
muhimu kufanikisha mkakati wa Kilimo Kwanza na uendelezaji wa ukuaji wa
kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) mkoani Morogoro.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde
la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja wilayani Kilombero mkoani
Morogoro wakati akizungumzia tatizo la miundombinu katika kivuko cha Mto
Kilombero hivi karibuni.
Alisema mkakati wa 'Kilimo Kwanza' utafanikiwa kama juhudi
zitazingatiwa za kuwepo kivuko chenye uhakika katika Mto Kilombero
kutokana na kivuko kilichopo kutokuwa na uwezo mkubwa wa kupitisha
mizigo kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
“Kivuko hiki kimekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wananchi wa maeneo
haya na hasa katika bonde la mto kilombero, kwa hiyo kinachohitajika ni
kuweka mkakati wa dhati wa kuhakikisha kuwa kunakuwa na mpango wa muda
mrefu wa kuondokana na tatizo lililopo sasa la kivuko,” alisema Masanja.
Aliongeza kuwa ili kuendana na dhana ya Kilimo Kwanza ni lazima pawepo
na njia mbadala ya kuondoa shida iliyopo kwa sasa, na kusisitiza kuwa
njia pekee ya kuondokana na adha iliyopo ni kuwa na daraja katika eneo
hilo.
“Kwa sasa mamlaka imejikita katika kupanua maeneo kwa ajili ya
uwekezaji, hivyo ni vema daraja likaboreshwa ili kuweza kuwavutia
wawekezaji wengi kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo katika bonde la
mto kilombero,” alisema Masanja.
Kwa sasa wawekezaji ambao tayari wamejitokeza ni wale wanaolima mpunga
katika shamba la Mngeta huku mafanikio yakionekana kuwa mazuri kutokana
na wananchi wa maeneo jirani kufaidika na uwekezaji mkubwa uliopo katika
shamba la Mngeta.
Katika kutekeleza azma hiyo ya kuwa na kivuko cha uhakika ama mpango wa
muda mrefu wa ujenzi wa daraja ili kuwavutia wawekezaji tayari RUBADA
walikutana na wadau mbalimbali katika sekta ya kilimo ili kuona
uwezekano wa kutatua tatizo hilo.
“Tulikubaliana kuwa tushirikiane pamoja na watoa maamuzi ili tuweze
kujenga daraja katika eneo hili na kutekeleza mkakati mzima wa kilimo
kwanza,” alisema Masanja.
Alisema maazimio mengine katika kikao hicho ni uwezekano wa taasisi za
serikali kushirikiana na sekta binafsi kuona uwezekano wa kuleta kivuko
kipya au kujenga daraja katika eneo hili la Mto Kilombero.
No comments:
Post a Comment