Na Yusuph Mussa, Tanga
MKUU wa Mkoa wa Tanga, Bi. Chiku Gallawa, amewataka wanasiasa na wataalamu kwenye mikoa ya Tanga na Mbeya hasa wabunge na madiwani kuenzi mradi wa mama na mtoto ambao utawawezesha kujifungua salama.
Aliyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwawezesha akina mama wajawazito wasio na uwezo wa kupata matibabu chini ya utaratibu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), kwa mikoa ya Mbeya na Tanga.
Mradi huo ambao unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW) kwa kushirikiana na NHIF. Uzinduzi huo ulishirikisha wakuu wa Wilaya, wabunge, wenyeviti, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine mkoani Tanga.
"Kupitia mradi huo kundi la akina mama wajawazito hasa wale wa kipato cha chini watakuwa wanufaika wakubwa. Sote ni mashahidi wa jinsi wanawake wa vijijini wanavyohangaika kufikia huduma za uzazi," alisema.
Bi. Gallawa alisema bila kuongeza wanachama wa CHF wasitarajie mapato kupanda kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati. Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Emmnuel Humba, alisema baadhi ya wafadhili wamevutiwa kusaidia wajawazito vijijini ili wapate huduma za afya.
"Mradi huu utawaisaidia akina mama kwenye wilaya nne na kata 97. Mpaka sasa fomu 12,000 zimesambazwa kwenye wilaya nne na akina mama 600 wamejiandikisha na kuanza kupata huduma,"alisema.
Mwakilishi wa KfW kutoka Ujerumani Dkt. Kai Gesing, alisema alifanya kazi miaka ya 1990 nchini kwenye mikoa ya Lindi na Mtwara aliona mwenyewe wanawake wa vijijini walivyokuwa wanateseka kupata huduma hasa za uzazi, hivyo wameshawishika kusaidia huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment