22 February 2012

Mazinde yataka mikopo isitolewa kwa ubaguzi

Na Yusuph Mussa, Lushoto

MKUU wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary's Mazinde Juu, iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga, Mtawa Evetha Kilamba ameiomba Serikali iepuke kutoa mikopo kwa ubaguzi kwa kuwapa wanafunzi waliosoma shule za Serikali pekee.

Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya 15 ya kidato cha sita ya shule hiyo na kuongeza kuwa Serikali itanue wigo kwa kuwapa hata wanafunzi waliosoma shule binafsi, kwani na wao wanahitaji mikopo hiyo.

"Tunaishukuru Serikali yetu ya Tanzania kwa kuwakopesha wanafunzi wanaojiunga na elimu ya juu. Tunaomba kwa heshima Serikali itoe mikopo kwa wanafunzi wote wanaojiunga na elimu ya juu bila kuangalia kama huyu ametoka shule ya binafsi au ya Serikali.

"Sisi kama Sekta binafsi tunajitahidi kutoa elimu bora kwa Watanzania bila kuangalia ametoka wapi. Pia tunaomba Wazazi pamoja na Serikali kutusaidia kujenga nyumba tatu za walimu, tayari wazazi walisaidia kukamilika kwa nyumba tatu bado tatu," alisema Mtawa Kilamba.

Mtawa Kilamba alieleza siri ya shule yake kufanya vizuri kitaaluma ikiwemo matokeo ya kidato cha nne mwaka jana, ambapo wamefanikiwa kukamata nafasi ya saba kitaifa, huku akieleza nidhamu ni kipaumbele chao cha kwanza mwanafunzi kufanya vizuri.

"Walimu wa shule hii wanajituma kufuatilia suala la nidhamu na taaluma. Pia wanapenda kazi yao ya kuwaelimisha vijana hawa. Lakini pia wazazi na walezi wanaosomesha watoto wao hapa ni matajiri wa fadhila kwa kutupa misaada mbalimbali," alisema Mtawa Kilamba.

  

No comments:

Post a Comment