13 February 2012

Miundombinu Soweto iboreshwe

kupunguza migogoro

Na Esther Macha,

HIVI karibuni kumeibuka migogoro isiyo kuwa na suluhu katika maeneo mbali mbali nchini ambayo imekuwa ikisababisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo kushindwa kufanyika kwa wakati .

Nasema hivi kwa sababu, inapotokea kazi zinazohusu maendeleo hushindwa kuendelea kutokana na watekelezaji wake kugoma wakidai haki zao za msingi ili waweze kupatiwa.

Lakini hali hiyo siku zote imekuwa tofauti ambapo serikali imekuwa ikifumbia macho malalamiko hayo pasipo kuyafanyia kazi na kubaki kutoa ahadi zisizokuwa na utekelezaji ndani yake.

Ili kuweza kuona kuwa, haki inatendeka migomo pekee ndiyo imeonekana kutawala karibu nchi nzima kwa kuona ni suluhu ya kumaliza matatizo hayo si kweli kwamba matatizo hayo yanaweza  yanaweza yakaisha kwa njia hiyo.

Katika kuhakikisha hayo yanafanikiwa wafanyabiashara wa soko la Soweto na Halmshauri ya jiji la Mbeya wamekuwa na mgogoro wa muda mrefu ambao licha ya  kugoma bado uongozi  haukutaka kutimiza mahitaji yao.

Wafanyabiashara hao wamekuwa wakilalamikia hatua ya kupandishiwa ushuru wa vibanda na meza pasipo kuboresha miundo mbinu ya soko hilo iliyochakaa na kukatisha tamaa kutokana muonekano wakeo.

Katika malalamiko yao, wafanyabiashara wamasema kuwa, awali walikuwa wakilipa ushuru wa sh.200 lakini baadaye ilipanda hadi sh.300 na kusababisha wahoji upandaji huo wakati hakuna maboresho ya miundo mbinu katika soko.

Ninachojiuliza ni kwanini halmashauri washindwe kutimiza malalamiko ya wafanyabiashara wakati ushuru unakusanywa kusaidia kutatatua matatizo hayo.

Kinachoonekana kushangaza kuhusu mgogoro huu ni kutokana uongozi wa halmshauri na wafanyabishara ambapo awali walikubaliana kwa pamoja kuwa, itaboresha miundo mbinu hiyo lakini hali hiyo imekuwa tofauti na kusababisha mgomo.

Kama walikubaliana kuboresha miundo mbinu mara baada ya kupandisha ushuru huo iweje tena wabadilike na kuanza kutoza ushuru huo pasipo kufanya matengenezo ya miundo mbinu hiyo?

Ninachokiona hapa ni propaganda  kutawala zaidi kuliko kuboresha soko hilo ambalo hata ukiangalia kwa macho muonekano unaonyesha kuwa ni mbaya hata kwa madhari yake ambayo yanaonyesha kuchoka licha ya kukusanya ushuru kila siku.

Lakini kwanini siasa zitawale kiasi hiki katika migogoro, hili suala la ni dogo sana kulimaliza lakini limeendelea kuwa kubwa lakini halmshauri imebaki kuwa na ahadi zisizokuwa na utekelelezaji .

Wafanyabishara wameshindwa kusaidia  kumaliza mgogoro huo kwani, kitendo cha kugomea ushuru huo ni kuzoretesha biashara zao.

Natambua kuwa, wana wajibu wa kulalamikia ushuru huo lakini pia wanatakiwa kuangalia maslahi ya biashara zao kwani sidhani kama wanafanya migomo ya kutofungua masoko kwa kuwakomesha viongozi.

Nilifikiri kwamba, wangeendelea na biashara na kuweka msimamo wa pamoja kutolipa ushuru huo mpaka pale watakapoboreshwa miundo mbinu hiyo.

Ni kwamba kitendo cha wafanyabiashara hawa kugoma ni kuharibu ni kujirudisha nyuma kwa kuwa,  wengine wana bidhaa ambazo ni rahisi kuharibika na wengine wana mikopo inayotakiwa kurejeshwa.

Wanatakiwa kutafakari kwa makini suala hili kwa kuangalia madhara yake, wengine wamegoma bila kufahamu wanachofanya na madhara yake kwa baadaye.

Ifike kipindi watanzania tujifunze kuhusu migomo kwa kuwa, toka serikali ilipopiga marufuku nchi nzima maandamano kilichobadili sasa ni migomo ambayo imekuwa ikiibuka kila kukichao pasipo kupatiwa suluhu.

Nashauri wahusika wakuu  wajaribu kukaa pamoja na kuyamaliza,  migomo sio jibu kwani tumeshuhudia walimu wakigoma mara kadhaa lakini wamekuwa wakiishia kudanganywa na kusitisha migomo hiyo.

Nafanyabiashara hawa wana uchungu wa fedha zao ambazo wanapata kwa kutumia jasho lao hivyo, wanataka zitumike kuboresha maeneo yao na kuvutia wateja wao.

Nawaomba  wafanyabiashara warudi katika biashara zao ili wasiweze kupata hasara zaidi kwani kitendo cha kufunga biashara peke yake kwa siku nzima ni hasara tosha.

Pia, halmshauri inatakiwa kuwa sikivu kwa wananchi kama fedha ipo waboreshe miundo mbinu ili kuzuia migogoro mingine.

Katika mgomo huo  Meya wa Jiji la Mbeya, Bw.Athanasi Kapunga alisema uamuzi wa kupandisha ushuru hautasitishwa kwa sababu makubaliano hayo yalifanyika baina ya uongozi soko na halmashauri.

Kauli za hiyo ilikuwa mwiba wa wafanyabiashara hao kwa kuhoji kuwa,  wanachosimamia hapo ni kupanda kwa ushuru tu na si kuangalia ubovu wa miundo mbinu ya soko.

Viongozi wa jiji wamekosea kauli hiyo ya kuweka maslahi mbele badala ya kuboresha soko.

Wanatakiwa kufahamu kuwa, wapewa dhamana ya kutatua migogoro  inayotokea katika jamii.

Mgogoro huu  umekuwa wa muda mrefu bila sababu ya msingi kuwepo wakati viongozi wenye dhamana wapo. Kinachokuwa kigumu kutekeleza malalamiko haya nini hasa wakati suala hilo linaweza kutatulika mapema bila hata kuwepo migogoro .

Lakini pia tumekuwa tukishuhudia wanasiasa  wengi wakiona sehemu yenye migogoro kujipachika kuwa ndo ajenda kuu ya kuzungumza kila mara pasipo kufanya utekelezaji.

Kama kweli wanasiasa wana uchungu na wafanyabiashara iweje iwe ngumu kulimaliza hili la ushuru?

Ni wakati wa kuonesha kwa vitendo mliyoahidi kwa wananchi wenu, mgogoro huu umalizwe na wananchi na watendaji.

No comments:

Post a Comment