09 February 2012

Mgomo wa madaktari: Wanaharakati waingia mitaani, Bunge latoa tamko

*Mbatia amshangaa JK, wabunge wajionea maafa Muhimbili
Na Waandishi Wetu

SAKATA la mgomo wa madaktari, jana limeendelea kuchukua sura mpya baada ya wanaharakati kuandamana jijini Dar es Salaam ili kuishinikiza Serikali kuwalipa madaktari wakiamini hatua hiyo itawafanya warejee kazini kuokoa maisha ya wagonjwa.

Katika maandamano hayo, wanaharakati hao walienda mbali zaidi na kumshukia Spika wa Bunge, Bi.Anne Makinda, wakidai amekuwa akiendesha vikao vya bunge wakati Watanzania wanaendelea kufa kutokana na mgomo huo.

Wanaharakati hao walijikusanya katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi eneo la daraja la Salender na kuanza kutoa dukuduku lao, huku askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wakishuhudia.

Wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali, waliitaka Serikali hadi kufikia leo, iwe imetafuta suluhu ya mgomo huo vinginevyo watahamasisha maandamano makubwa nchi nzima.

Miongoni mwa mabango hayo yalikuwa na ujumbe unaosema, “Rais Kikwete watu wanakufa uko wapi, viongozi mkiugua mnakimbizwa India kutibiwa na wabunge mnatusaliti'.

Mabango mengine yalisomeka “Wananchi wanakufa, Serikali yetu inawajibika kwa nani, Waziri wa Afya unahusika na afya za akina nani wakati watu wanakufa na mnatuua”.

Akifikisha ujumbe wa maandamano kwa niaba ya wanaharakati, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt.Hellen Kijo Bisimba, alisema lengo la maandamano hayo ni kufikisha ujumbe kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye amekuwa kimya wakati wananchi wanaendelea kufa.

“Jana tulikuwa Muhimbili na hospitali nyingine za Wilaya, tuligundua kuwa Watanzania wengi wana matatizo makubwa, maiti zimezagaa Muhimbili kwa sababu hakuna daktari wa kusaini ili ziondolewe wodini.

“Hatujui tunaelekea wapi na kiongozi wa nchi yupo kimya, muda wote yupo nje ya nchi katika ziara bila kujali wananchi wake wanakufa, tumechoka na propaganda,” alisema Bi.Bisimba.

Aliongeza kuwa, Bi.Makinda na Naibu wake, Bw.Job Ndugai, wameendelea kuendesha vikao vya bunge na kuchukua posho wakati Watanzania wanapoteza maisha kila kukicha.

“Kimsingi Bi.Makinda anatudhalilisha wanawake wa nchi hii kutokana na ukimya wake mbali ya nafasi aliyonayo, tumueleweje au tumuweke katika kundi gani,” alihoji Mkurugenzi Mkuu wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya.

Tume yaanza uchunguzi
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, imeanza uchunguzi ili kubaini Serikali imehusika kwa kiwango gani kuvunja ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayompa  mwananchi haki ya kuishi.

Uchunguzi uliofanywa na Majira, umebaini kuwa uchunguzi huo ulianza tangu kuanza kwa mgogoro huo ikiangali maeneo ya utoaji huduma za matibabu jinsi yalivyoathiri wagonjwa na baadaye kutoa ripoti yake kwa Serikali.

Inadaiwa kuwa, uchunguzi huo unafanywa na Maofisa watano wa tume hiyo ambao hivi sasa wapo katika hatua ya mwisho kuangalia idadi ya vifo vilivyotokea tangu mgomo huo uanze.

Akizungumza na Majira, mmoja wa maofisa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema Serikali na madaktari hawajawatendea haki wananchi.

“Wananchi wana haki ya kuishi, ibara ya 8 (1) ya katiba ya nchi, inasema wananchi ndiyo msingi imara wa nchi," alisema na kuongeza kuwa, katika uchunguzi wao, wamebaini kinachoendelea MNH ni uvunjifu wa haki za binadamu hasa kwa kuzingatia kuwa, wananchi wana haki ya kuishi na kupatiwa matibabu.

Wakati tume hiyo ikifanya uchunguzi huo, jana Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, ilitembelea hospitalini hapo kujionea hali halisi.

Ingawa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bi.Magreth Sitta, alisema hawawezi kuzungumza lolote kuhusu walichokiona Muhimbili hadi wafikishe ripoti bungeni, wajumbe wa kamati walishuhudia mateso wanayopata wagonjwa.

Mbunge wa Kigamboni Dkt. Faustine Ndungulile, alikiri kuwa hali ni mbaya ndiyo maana wamefika hospitalini hapo kujionea wenyewe.

Kamati ya Bunge
Kamati hiyo ilitembelea wodi ya watoto, wanawake, Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) na wodi ya Sewahaji ambako walijionea mdororo wa huduma za matibabu baada ya kusitishwa huduma.

Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Lucy Nkya, alisema kamati ya bunge ilitumwa kufanya mahojiano na pande zote mbili ili waweze kutoa tamko kuhusu hali hiyo.

“Madaktari wanapaswa kutambua wao ni sehemu ya Taifa hili hivyo ni muhimu wakaonesha uzalendo kwa kuzingatia viapo vyao, mimi bado naunga mkono msimamo wa Serikali wa kuwataka warudi kazini kwani madai yao yanazungumzika,” alisema Dkt. Nkya.
Mbatia anena
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw.James Mbatia, amemtaka Rais Kikwete, kumwajibisha Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Haji Mponda na achukue hatua za dharura kuwalipa madai yao madaktari waliogoma ili waanze kazi haraka.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Mbatia alisema mgogoro huo usingefikia hatua hiyo kama si jeuri ya Serikali iliyofanywa na Dkt.Mponda kwa kupuuza madai yao.

"Kupanga ni kuchagua, Serikali ichague uhai wa wananchi wake au vifo, kama chenji ya rada imerudi ipelekwe kulipa madaktari," alisema Bw.Mbatia.

Aliongeza kuwa, msafara wa rais unatembea na magari zaidi ya 20 barabarani huku wananchi wakifa kwa kukosa huduma za matibabu kutokana na mgomo wa madaktari wanaodai maslahi yao.

"Rais Kikwete atoe tamko la kutatua mgogoro huu kwa kusimamisha moja ya miradi ya Serikali na mabilioni ya fedha hizo ziwalipe madaktari waendelee na kazi," alisema.

Aliongeza kuwa, Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii iliyokuwa ikifuatilia suala hilo, imetumia pesa nyingi za walipa kodi ambao wanapoteza maisha kwa kukosa huduma.

"Kiongozi wa nchi ana mamlaka ya kusimamisha mradi wa ujenzi wa nyumba za Serikali, barabara au uwanja wa ndege na fedha hizo zikaokoe wagonjwa kwa kuwalipa madaktari,"alisema.

Bunge latoa tamko
Wakati hayo yakiendelea, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limesema, mgomo wa madaktari bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), unapaswa kujadiliwa kabla ya kuahirishwa kwa mkutano wa Bunge unaoendelea mjini Dodoma vinginevyo wabunge wataonekana watu wa ajabu.

Naibu Spika, Bw.Job Ndugai, aliyasema hayo bungeni jana baada ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Bw.Peter Serukamba, kuomba mwongozo wa spika na kutoa hoja ya kulitaka bunge lisimamishe shughuli zake ili kujadili suala hilo.

"Mheshimiwa Serukamba amesimama hapa kuomba mwongozo
kwa kutumia Kanuni ya 47 (1) inayosema kuwa, Mbunge yeyote anaweza kusimama baada ya kipindi cha maswali na majibu na kutoa hoja ili Bunge liahirishe shughuli zake ili kujadili jambo muhimu kwa maslahi ya Taifa," alisema.

Kutokana na hoja hiyo, Bw. Ndugai aliitaka Kamati ya Uongozi ya Bunge ikutane na Spika wa bunge, Bi.Anne Makinda, kushauriana hatua za kuchukua ili kushughulikia mgomo huo.

Kwa upande wake, Bw.Serukamba alisema mgomo huo umezidi kukua siku hadi siku na kusababisha Watanzania wengi kupoteza maisha kwa sababu ya kukosa matibabu.

"Kama bunge linashindwa kuchukua hatua ya kuishauri Serikali ili kumaliza mgomo huu, nini kifanyike ili kunusuru hali hii, mgomo umedumu kwa wiki ya pili sasa.

"Kama bunge litashindwa kujadili suala hili kama dharura kwa hofu ya kuingilia mihimili mingine, litaonekana la ajabu, lisilojali maslahi ya Watanzania wanaowawakilisha," alisema.

Bw.Ndugai alisema tangu kuanza kwa Bunge la sita, suala hilo limekuwa likiombewa mwongozo na wabunge akiongeza kuwa, hali ilivyo sasa mgomo huo umefikia hatua ya kuwa janga la kitaifa.

"Hili suala kwa sasa linakidhi vigezo vyote vya dharura ndio maana nimelazimika kuitisha kamati ya uongozi iweze kumshauri Spika wa Bunge, hatua za kunusuru hali hii,"alisema.

Aliongeza kuwa, kwa mujibu wa katiba bunge ndio chombo chenye madaraka ya kusimamia na kuishauri Serikali.

"Hapa lazima tukubaliane, hauwezi kuwa mshauri mzuri kama huna taarifa kamili ya jambo unalotaka kushauri, kutokana na unyeti wa jambo lenyewe, si busara kulinyamazia kimya,"alisema Bw.Ndugai na kuwaomba madaktari waliogoma, kuwa na moyo wa subira pamoja na kurejea kazini ili kuokoa maisha ya Watanzania wakati Serikali ikishughulikia madai yao.

Hospitali ya Rufaa Mbeya
Huko mkoani Mbeya, madaktari 17 waliopo katika Hospitali ya Rufaa mjini Mbeya, hawajajiunga na mgomo wa madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ili kuishinikiza Serikali isikilize madai yao.

Jana madaktari hao waliendelea na kazi kama kawaida kutokana na kile kilichoelezwa kuwa, hali hiyo imechangiwa na huruma waliyonayo kwa wagonjwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dkt.Hamphrey Kikwelu, alisema miongoni mwa madaktari hao ni pamoja na wakuu wa idara.

Imeandikwa na Grace Ndossa, Rehema Maigala, Peter Mwenda, Anneth Kagenda, Pendo Mtibuche na Charles Mwakipesile.

1 comment:

  1. Madaktari wana haki ya kudai maslahi yao kama watumishi wengine wa serikali ila jambo ambalo silielewi ni kwanini uue mtu yaani mgonjwa ili mtu mwingine akusikilize wewe hapo sijaelewa. Kumbukeni madaktari na Serikali roho za watu mliowaua kwa mgomo wenu zitzwalilia kwa Mungu maisha yenu yote!

    Mnachokifanya ni sawa na kuwaambia polisi na askari wa JWTZ waache kutulinda tuuliwe na majambazi mpaka madai yao yatakaposikilizwa!

    Hivi kweli busara zooote zimekosekana mpaka muamue kuua watanzania wenzenu kwanza?

    Upo mgomo mwingine wa waalimu ambao umekua ukiendelea miaka mingi sana nao wanaua taifa kimya kimya kiulaini bila kelele na mtu, kifo cha ujinga cha Taifa hili tutakiona mika hamsini ijayo! nao ni mwendelezo wa laana kama hii ya Kugoma.

    Ni vizuri suala hili tukaliangalia kikatiba yaani yale makundi yanayohudumia watanzania wengi zaidi kama wauguzi, madaktari, waalimu na Polisi maslahi yao yawekwe kikatiba na yasimamiwe na bunge ili serikali isiwadhulumu kwani ndiyo makundi yanayowahudumua watanzania wengi zaidi kila siku!

    Poleni watanzania kwani Serikali yetu na madaktari wamekosa busara kunusuru maisha yetu!

    ReplyDelete