Na Amina Athumani
CHAMA cha Netiboli Tanzania (CHANETA) na Chama cha Netiboli ZANZIBAR vimekubaliana kuiingiza kambini timu ya Taifa ya mchezo huo 'Taifa Queens' Februari 20 mwaka huu kujiandaa na michuano ya Afrika ya mchezo huo.
Makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha pamoja kilichohusisha vuiongozi wa CHANETA, na CHANEZA kilichofanyika juzi jijini Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa CHANETA, Rose Mkisi alisema wamekubaliana kutoa wachezaji 30 ambapo CHANEZA yenyewe itatoa wachezaji 10 na CHANETA wachezaji 20 ambao watakaa kambini jijini Dar es Salaam.
Alisema kambi hiyo ni maalum kwa ajili ya michuano hiyo ya Afrika ambapo Tanzania imepewa kibali na Shirikisho la Kimataifa la mchezo huo (IFNA) kuandaa mashindano hayo yaliyopangwa kufanyika Mei 8 mwaka huu.
Alisema tayari wameshatuma barua kwa nchi zinazotakiwa kushiriki mashindano hayo ambapo wanategemea kupokea zaidi ya timu 16 kutoka katika nchi za ukanda wa Afrika.
Alisema mashindano hayo yataiwezesha Tanzania kupanda viwango vya IFNA ambavyo kwa sasa inashika nafasi ya 22 kimataifa na nafasi ya tatu katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkisi alisema wameamua kuweka kambi ya wachezaji hao mapema ili timu hiyo iweze kufanya vizuri katika michuano hiyo mikubwa kwa mchezo huo barani Afrika.
Kwa mara ya kwanza Tanzania ilipewa kibali cha kuandaa mashindano hayo mwaka 2009 ambapo hii itakuwa ni mara ya pili kwa Tanzania kuandaa mashindano hayo.
No comments:
Post a Comment