01 February 2012

Bayport yatoa msaada wa vitabu Kigoma


Na Mwali Ibrahim

TAASISI ya kifedha ya Bayport kupitia  kampeni yake ya 'Bayport Books for Schools' jana imezindua rasmi kampeni hiyo kwa  kutoa vitabu vya darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Boma iliyoko Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma.


Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Meneja Masoko na Uhusiano wa Bayport Bw.Ngula Cheyo ilisema kuwa Bayport itatoa vitabu 120 kwa kila shule za msingi katika Wilaya hiyo kwa lengo la kusaidia kukuza kiwango cha elimu kwa watoto hao.

Alitaja aina ya vitabu watakavyotoa kuwa ni kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na kingereza pia vitabu 80 kwa kila  shule za sekondari kwa masomo ya Sayansi, Hisabati na atlasi 2 kwa kila shule za wilaya hiyo.

"Bayport imeamua kutoa msaada wa vitabu kwa darasa la kwanza na kidato cha kwanza kwa kuwa tunaamini kumpa mtoto mwamko wa elimu ni lazima kumjengea msingi madhubuti  mapema  katika elimu yake ya chini yaani darasa la kwanza na kidato cha kwanza," alisema.

Bayport kupitia huduma hiyo imedhamiria kutoa vitabu kwenye shule 20 katika wilaya 20 za Tanzania bara ili kuweza kuboresha elimu katika shule hizo na kupunguza adha ya kukosekana kwa vitabu vya kusomea.

Wakati huo huo Bayport ilizindua rasmi tawi lake  Kibondo ambalo ni tawi la 60 miongoni  mwa matawi yake yaliyoenea.


No comments:

Post a Comment