16 January 2012

Zambia yatabiliwa makubwa CAN 2012

JOHANNESBURG,A.Kusini

MCHAMBUZI wa masuala ya soka katika televisheni ya  Super Sport, Thomas Kenaite, amesema kuwa timu ya Taifa za Zambia ina nafasi ya kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya fainali za Mataifa ya Afrika (CAN) 2012.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa ndani pamoja na mashabiki wa soka hawakubaliani na mchambuzi huyo kuhusu kutwaa kombe kwa wakati huu, lakini wengine wana uhakika kwamba Zambia inaweza kufika mbali na kuwashangaza wengi.

Kenaite alisema kwa sasa Chipolopolo inaonekana kuwa ni nzuri zaidi kuliko iliyofikia robo fainali ya michuano iliyofanyika nchini Angola mwaka 2010.

Mchambuzi huyo alisema kuwa endapo Zambia, itafanikiwa kuipiku  Senegal, huenda ikatwaa taji hilo kwa mara ya kwanza.

Alisema kukosekana kwa vigogo vya soka barana Afrika kama  Nigeria, Cameroon na Misri kunaipa Zambia nafasi ya kutwaa ubingwa huo.

Kenaite alisema kuwa  Zambia haipaswi kuihofia  Ivory Coast kutokana na kwamba timu hiyo inakabiliwa na migogoro lakini akaonya kuwa Senegal inaweza kupeperusha nafasi ya Chipolopolo kutwaa taji hilo.

No comments:

Post a Comment