27 January 2012

WAKAZI WA DAR WALIA NA MFUMUKO WA BEI.

Na Rachel Balama

WANANCHI wa maeneo mbalimbali Jijiji Dar es Salaam wamesikitishwa na mfumuko wa bei za bidhaa muhimu kwani hali  hiyo inawaweka katika wakati mgumu


Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wananchi hao walisema kuwa wamekuwa wakiishi  katika mazingira magumu kutokana na kutokuwa na kipato cha kukidhi mahitaji yao.

Asha Ramadhani, Mkazi wa Kiwalani, alisema kuwa kwa kutokana na hali hiyo amejikuta akilazimika kula milo miwili kwa siku kutokana na kushindwa kumudu gharama.

"Kutokana na kipato changu kuwa kidogo, sasa nakula mlo mmoja kwa siku jambo ambalo watoto wangu wanashindwa kuvumilia," alisema.


Naye, Salma Ramadhani, alisema kuwa katika Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam kumekuwa na ongezeko la bei za vyakula mfano, mfuko mmoja wa sukari wa kilo 25 unauzwa sh 80,000 kwa bei ya jumla kutoka sh 40,000 ikiwa imepanda mara dufu huku kilo moja ikiuzwa kati ya sh. 2,000 hadi 2,500.

Alisema kwa upande wa masoko kama Tandika, Kariakoo na Tandale taarifa inaonyesha bei ya vyakula imepanda kwa kasi katika miezi mitatu iliyopita. Kwa sasa gunia moja la mchele linanunuliwa kati ya sh.250,000 hadi 300,000 kutoka sh 100,000 hapo awali, Wakati kilo moja ya mchele kwa sasa ni kati ya sh. 2,000 hadi 2,500.

Kwa upande wa mchele wa kitumbo ambao jamii kubwa ya watanzania wanaoishi maisha magumu wamekuwa wakiutumia kwa sasa huuzwa kwa kiasi cha Sh 1600 hadi 1800 kwa kilo tofauti na awali mchele huo ulikuwa ukiuzwa kwa Sh 1000 hadi 1300 ambapo ulikuwa ukitumiwa na wafanyabiashara wa vitumbua.

Wananchi hao wameiomba  serikali kusimamia  kwa makini tatizo la mfumko wa bei sambamba na ongezeko la bei ya umeme ili shughuli  za uzalishaji ziendelee kwa nia ya kuwanusuru wananchi hasa kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment