01 February 2012

KIPA namba moja wa Yanga Yaw Berko atarejea kikosini

Na Amina Athumani

KIPA namba moja  wa Yanga Yaw Berko atarejea kikosini leo kuongeza nguvu baada ya kuwa majeruhi kwa muda mrefu.

Berko alishindwa kufanya mazoezi kwa muda mrefu na wachezaji wenzake baada ya kuumia  goti  kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi iliyokuwa ikifanyika visiwani Zanzibar.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Yanga Luis Sendeu alisema Berko atajiunga na wachezaji wenzake leo na kufanya mazoezi baada ya kutoonekana katika kikosi hicho kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

Alisema wachezaji wengine Nurdin Bakari, Rashid Gumbo pamoja na Godfrey Bony ambao pia walikuwa majeruhi kwa sasa wote wapo katika hali nzuri na wanaendelea na mazoezi kama kawaida.

Alisema kurudi kwa kipa huyo kutaongeza zaidi uhai katika timu hiyo ambayo kwa sasa inajiandaa na mechi dhidi ya Zmalek ya Misri mechi itakayochezwa Februari 18 mwaka huu katika uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Alisema wiki mbili kabla ya mechi hiyo timu hiyo itahamishia kambi yake jijini Mwanza kwa ajili ya kujifua zaidi na kwamba kama kutakuwa na mabadiliko yoyote watatoa taarifa.

Sendeu alisema pia ili kuhakikisha wanaiondoa Zamalek timu yao itaendelea kuzitumia mechi za ligi kuu Tanzania bara kama sehemu ya maandalizi ya kujiweka vizurui zaidi kuikabili Zamalek.

Mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Zamalek itachezeshwa na waamuzi kutoka Ethiopia ambapo itakuwa ni mechi  namba 7 ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Bamlack Tessema kuwa mwamuzi wa kati kwenye mechi hiyo wakati waamuzi wasaidizi ni Yilma Knife na Mussie Kindie.

Mwamuzi wa akiba atakuwa ni Waziri Sheha kutoka Tanzania na Kamishna wa mchezo huo ni Charles Kafatia wa Malawi.




No comments:

Post a Comment