27 January 2012

SERIKALI IUNDE CHOMBO CHA KUDHIBITI BEI -GDSS

Na Rose Itono

WADAU wa semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wameitaka serikali kuwa na chombo maalumu cha kudhibiti bei za bidhaa ili kuwawezesha wananchi wa kumudu gharama za maisha.

Wakizungumzia kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania,mfumuko wa bei na hali ngumu ya maisha na athari zake kwa wanawake na makundi yaliyopo pembezoni katika viwanja vya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Dar es Salam juzi  walisema kutokuwepo kwa chombo cha kudhibiti hali hiyo  kunachangia mfumuko wa bei za vyakula.

Mwakilishi wa wanawake hao Bi. Anna Sangai alisema kama chombo hicho kitaundwa  kitasaidia kusimamia bei za bidhaa kama ilivyo Mamlaka  ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ambao ambayo inasimamia  bei za nishati na maji.

Bi.Sangai  alisema kuwa,hali ya serikali kutothamini watu wake waliopo katika jamii inachangia kwa kiasi kikubwa kuwepo na matabaka ya walionacho na wasionacho.

"Ukweli ni kwamba kumekuwa na ongezeko kubwa la matabaka kwa watu walionacho na wasionacho,"alisema Bi. Sangai.

Aliongeza kuwa hali hii imewafanya watu hasa wale wa pembezoni na wenye kipato cha chini kulazimika kula milo miwili kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha.

Bw.Ahmed Nasoro mkazi wa Mabibo alisema kuwa, uchumi wetu umekuwa ukitumika katika shughuli za kisiasa zaidi kuliko shughuli za kijamii.

Alisema hii ni kutokana na kwamba bajeti kubwa ya serikali inaelekezwa zaidi katika shughuli za kisiasa kuliko za kijamii.

Naye Bi.Evin Mafem mkazi wa Kimara alisema ni vema serikali ikaandaa utaratibu wa kuzungumza na wananchi wake hasa wale pembezoni ili kujua matatizo yanayowakabili ili waweze kuyafanyia kazi.

Aliwaka wadau mbalimbali kuendelea kusimama imara kupigania haki zao ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi, kuyafanyia kazi masuala yote yanayoikabili nchi hii ikiwemo hili la kushuka kwa thamani ya shilingi.


2 comments:

  1. Kama vile ilivyo EWURA serikiali iunde tume ya kudhibiti bidhaa za chakula zitakazojumuisha mchele,unga,sukari,maharage na mafuta ya kupikia.

    ReplyDelete
  2. Nendeni mkalime hivyo vyakula kama mnadhani kazi ya kulima ni rahisi.

    ReplyDelete