18 January 2012

Waigomea halmashauri wakitaka ipunguze ushuru

Na Esther Macha, Mbeya
Wafanyabiashara wa Soko la Soweto mkoani Mbeya jana waligoma kwa muda wa
saa tatu kwa madai ya kulalamikia Halmashauri ya Jiji la Mbeya
kuhusu kupunguza ushuru wa biashara.
Mgomo wa wafanyabishara hao ulianza majira ya saa moja za asubuhi na kudumu hadi saa nne asubuhi ambapo mara baada ya hapo, wafanyabiashara hao waliendelea na biashara zao kama kawaida.
Wakizungumza na Majira baadhi ya wafanyabishara wa soko hilo walisema, kupanda kwa kiwango cha ushuru kutoka sh. 200 hadi 500, hicho ni kiwango kikubwa ambacho hawawezi kukabiliana nacho kwa madai kuwa kipato chao ni duni.
Hata hivyo akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi wa jiji hilo, Bw.Juma Iddi alisema, mazungumzo kati ya uongozi wa soko na Serikali yanaendelea vizuri na kwamba atatolea ufafanuzi mara baada ya kikao kumalizika hivi karibuni.
Alisema, tayari uongozi wa halmashauri ya jiji hilo upo katika
kikao ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo linakwisha na watu wanaendelea na
shughuli zao kama kawaida.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Bw. Evans Balama alisema, jiji linapaswa kukaa na wafanyabiashara hao ili kufikia muafaka kwa ufafanuzi kuwa maamuzi hayo yasijekuwaathiri wateja.
Hata hivyo mgomo huo wa wafanyabiashara umekuja mara baada ya halmashauri ya jiji kupandisha ushuru kutoka sh.200 hadi sh.500, kwa wateja waliokuwa wakipanga bidhaa zao mezani na kwa vyumba kutoka sh. 15,000 hadi kufikia 65,000 licha ya soko hilo awali kukosa wateja.

No comments:

Post a Comment