18 January 2012

Ofisi ya madini mbioni kukamilika Singida

Na Thomas Kiani, Singida

WIZARA ya Nishati na Madini imekusudia kukamilisha jengo la ofisi ya madini Kanda ya Kati Singida ambalo litagharimu sh.milioni 870  hadi litakapokamilika mapema mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Kamishina Msaidizi wa madini katika kanda hiyo, Bw.Manase Mbasha zilieleza kuwa wizara imekusudia kujenga ofisi hiyo ili kuwa karibu na wachimbaji wote wa madini na kutoa huduma kwa haraka zinazotakiwa katika shughuli zote za madini kwa watu binafsi, kampuni na wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Bw.Mbasha alisema, ofisi hiyo ya Singida itasimamia utafiti, uchimbaji, utoaji wa leseni zote za madini na vibali ikiwemo kusimamia biashara za madini katika mikoa ya Dodoma, Tabora, Shinyanga na Singida yenyewe kwa kampuni kubwa na ndogo kutoka nje na ndani ya nchi
Alisema, ujenzi wa ofisi hiyo ambayo itakuwa karibu na ofisi ya Mkuu wa mkoa ilianza kujengwa mapema mwaka jana chini ya Mkandarasi ambaye ni M/S Gross Investment Ltd kutoka jijini Dar es salaam na inatarajiwa kumalizika ujenzi wake wakati wowote ili kuanza kutoa huduma.
Hata hivyo Mhandisi wa migodi kanda ya kati, Bw.Gabriely Senge katika taarifa hiyo alibainisha hasa madhumuni ya serikali kujenga ofisi hiyo Singida kwamba ni ili kuratibu maendeleo ya sekta na madini yote yanayopatikana katika mikoa hiyo minne.
"Kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata leseni, vibali, vifaa na mikopo pamoja na utaalamu wa uchimbaji na utafiti na uchenjuaji wa dhahabu katika migodi midogo ya madini hayo na maelekekzo ya soko zuri ukiwemo utunzaji mzuri wa mazingira," alieleza.
Mhandisi Senge alisema, kwa upande wa watu binafsi na kampuni ofisi itasimamia kutoa leseni na vibali kuendelea kutafiti na uchimbaji wa madini kwa mikoa hiyo.
Mbali na hayo alitaja madini yaliopo kanda ya kati kuwa ni pamoja na Almasi, Dhahabu, Urania, Shaba, Chuma, Zirkoni, Jasi, Mawe ya nakshi, madini ya ujenzi na madini mengineyo ya vito sambamba na madini ya chokaa na chumvi ambayo huwa yanapatika katika baadhi ya maeneo ndani ya mikoa hiyo.

No comments:

Post a Comment