17 January 2012

TOC yaishangaa BFT kuishupalia Dar

Na Amina Athumani

KAMATI ya Olimpiki Tanzania (TOC), inashangwa na Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT) kwa kushindwa kuuneza mchezo wa ngumi nchi nzima na badala yake kuishupalia Dar es Salaam pekee, wakati shirikisho hilo ni kongwe hapa nchini.

Akizungumza Dar es Salaam jana mjini Kibaha, Pwani wakati wa kufungua mafunzo ya makocha wa mchezo wa ngumi, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi alisema BFT ina kazi ya ziada kuueneza mchezo huo katika mikoa mbalimbali nchini kwani wanaonekana kuushupalia zaidi Dar es Salaam na hasa katika timu za Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Katika mafunzo hayo yanayoendeshwa na mkufunzi Josef Diof, aliyeteuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Ngumi za Ridhaa (AIBA), yanashirikisha makocha wa ngumi 25 kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Mafunzo hayo yalifunguliwa na Katibu huyo kwa niaba ya Rais wa TOC Gulam Rashid.

Bayi pia alisisitiza nidhamu kwa makocha hao na kusema ni jambo la muhimu kwa makocha wa ngumi kuzingatia kwa kuwa mafunzo hayo, yashirikisha walimu ambao watakuwa mfano kwa mabondia.

Alisema TOC haitavumilia utovu wa nidhamu katika shughuli zake inazoziandaa, kama ilivyowahi kufanywa mwaka jana na makocha hao katika kozi ambayo ilishindwa kufanyika awali, baada mkufunzi kutoka nchini Algeria kuingia mitini .

Bayi alisema mafunzo hayo, yalikuwa yafanyike mapema  mwaka 2010 lakini kutokana na BFT kusimamishwa uanachama na AIBA, baada ya wachezaji wa ngumi kukamatwa Mauritius kutokana na tuhuma ya dawa za kulevywa, walipokuwa wamekwenda kushiriki mashindano ya Afrika mwaka 2008.

BFT mara ya mwisho ilipata mafunzo kama hayo mwaka 1998 na 2002, lakini mafunzo mengine yamechukua muda mrefu kutokana  na kwamba TOC hupewa na IOC nafasi ya kuandaa mara kila mwaka.

No comments:

Post a Comment