17 January 2012

Kill Music Award yazinduliwa

Na Victor Mkumbo

KAMPUNI ya Bia Tanzania TBL, kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA), jana wamezindua rasmi mchakato wa kutafuta na kuwapa tuzo wasanii wa Tanzania waliofanya vizuri katika kazi zao za muziki kwa mwaka 2011.

Akizungumza Dar es Salaam jana katika uzinduzi huo, Meneja wa bia ya Kilimanjaro George Kavishe, alisema mwaka jana tuzo za Kill Music zilifanyiwa mabadiliko ambayo kwa mwaka huu yataendelezwa na kuboreshwa zaidi.

"Akademia ya tuzo za muziki Tanzania ni mkusanyiko wa wadau wa muziki kati ya 50 hadi 100, kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao huwekwa pamoja na kuchaguana hatimaye wanapatikana wateule(Nominees)," alisema.

Kavishe alisema kinyang'ang'anyiro hicho ni baada ya majaji, kujiridhisha kuwa washiriki waliopendekezwa wamekidhi vigezo vyote muhimu, ambapo utaratibu huo kwa mwaka huu unatarajiwa kufanyika Januari 27 na 28.

"Hatua ya pili ni majaji, ambao huwa na hatua muhimu na hupiga kura wakizingatia vigezo vya kiufundi zaidi na pia kuhakiki uteuzi wa washiriki, uliofanywa katika hatua ya awali kwenye akademia husika ikiwa ni pamoja na kura zilizopigwa na wananchi," alisema.

Kavishe alisema hutumia zaidi vigezo halali vinavyopatikana na mkusanyiko wa rekodi za wasanii zilizotoka kwa mwaka 2011, pamoja na mafanikio ambapo jopo hilo hujumuisha wadau wa tasnia ya muziki 15 na fainali za mwaka huu zitafanyika Aprili 15 mwaka huu.

Alisema hatua ya mwisho ni ya wapenzi wa muziki waliopiga kura hizo, hujumuishwa katika kuchagua washindi ambapo kwa shindano la mwaka huu kura za wapenzi na mashabiki wa wasanii, zitabeba asilimia 70 na kura za majaji itakuwa asilimia 30.

Meneja huyo alisema katika kufanikisha upapigaji kura kutakuwa na njia ya ujumbe mfupi kwa simu za mkononi, barua pepe, njia ya kujaza sehemu maalumu magazetini na vipeperushi.

Naye Mratibu wa tuzo kutoka BASATA, Luhaja Agm, alisema wasanii wa tuzo hizo hawana budi kuitumia nafasi waliyopata ili kujitangaza zaidi kimuziki.

No comments:

Post a Comment