18 January 2012

Arusha waomboleza kifo cha mdau wa maendele

Na Pamela Mollel, Arusha
OFISA Maendeleo ya Jamiii wa Manispaa ya Arusha, Bw. David Ndauka amefariki
dunia juzi jioni
kwa ugonjwa wa shinikizo la damu wakati akikimbizwa hospitalini kwa matibabu.
Bw.Ndauka kwa muda mrefu alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa mujibu wa taarifa za ndugu na jamaa wa karibu.
Akidhibitisha kutokea kwa msiba huo jana, Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha Bw.Estomih Chang'a  alisema, msiba huo ni wa kusikitisha kwani marehemu alifariki dunia ghafla jioni juzi wakati akikimbizwa hospitalini kwa Dkt. Urassa mkoani humo.
"Ni kweli, Bw.Ndauka amefariki jana (juzi) jioni kwa shinikizo la damu, ni ugonjwa aliokuwa nao kwa muda, na kwa bahati mbaya alifariki dunia wakati akikimbizwa hospitalini;
"Tumempoteza mtu muhimu sana, kwani yeye alikuwa ni mtaalamu aliyeisaidia halmashauri yetu kuunganisha vijana katika makundi na kuwasaidia kupata usajaili wa vikundi ambavyo kwa sasa tunavitumia vikundi hivyo kwa shughuli mbalimbali ili kuweza kupunguza wimbi la ajira kwa vijana," alisema.
Aliongeza kuwa marehemu kabla ya kukutwa na mauti alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Meru ambapo alikuwa akisomea shahada ya juu lakini kwa sasa taratibu za mazishi zinaendelea kwa kushirikiana na ndugu wa marehemu huko nyumbani kwake Kambi ya Chupa mkoani humo.
"Nimapema sana kusema wanazika lini, ila msiba huo upo nyumbani kwake Kambi ya Chupa na taratibu za mazishi zinaendelea tutawaarifu,"alisema Bw.Chang'a

No comments:

Post a Comment