16 January 2012

Nyilawila atamba pesa mbele, mataji nyuma

Na Mwali Ibrahim

BONDIA Karama Nyilawila ameibuka na kudai kitendo cha kunyang'anywa mkanda wake wa Ubingwa wa Dunia wa WBF, na waandaaji wa mashindano hayo hakimsumbui kwani yeye anachoaangalia ni pesa.

WBF hivi karibuni ilitangaza kumnyang'anya ubingwa huo kupitia kwa wasimamizi wa wao nchini, Shirikisho la  Ngumi za Kulipwa (PST), linaloongozwa na Rais, Emmanuel Mlundwa baada ya kutangaza kucheza pambano lisilo la ubingwa na Francis Cheka kitu ambacho hakitakiwi na WBF.

Akizungumza Dar es Salaam juzi, Nyilawila alisema hawezi kucheza pambano kwa kutafuta sifa bila kuwa na fedha kwani yeye anachoangalia zaidi ni maslahi.

"Kunyang'anywa ubingwa hakunitishi kama historia ya kuwa bingwa wa Dunia wa WBF mwaka juzi itabaki kuwa pale pale ingawa wameninyang'anya mkanda bila kupigwa, natafuta pesa sifa hazina nafasi kwangu kwani ubingwa wa Dunia naweza kuwania hata katika mikanda mingene," alisema Nyilawila.

Alisema amekaa kipindi kirefu bila kuwa na pesa na hata kupanda ulingoni sasa amepata sehemu ya kujikwamua hawezi kuipoteza nafasi hiyo kwani hata pesa ambazo angezipata huko ni ndogo kuliko anazozipata katika pambano lake na Cheka.

Alisema kwa sasa ameshapandisha uzito wake hadi kilo 75 ambao amesaini kucheza na Cheka ambapo ingekuwa vigumu kushusha haraka uzito huo hadi kufikia kilo 72 ambao alisaini katika ubingwa huo wa Dunia.

Aliongeza pambano lake na Cheka liko palepale na kwa sasa anaendelea kujifua na anaimani atashinda hata wakifika raundi ya mwisho.

Naye kwa upande wake Promota wa pambano hilo, Philemon Kyando alisema, maandalizi yanaendelea ambapo mabondia wote wapo katika hali ya kuushindani.

Aliwataja mabondia watakaosindikiza pambano hilo kuwa ni Maneno Osward 'Mtambo wa Gongo' akicheza na Nasib Ismail, Chaulembo Palasa na Seba Temba, Venance Mponji na Ibrahim Elask na Antony Mathias atazichapa na Juma Afande.

No comments:

Post a Comment