18 January 2012

Mwekezaji A to Z aomba wizara kuwapunguzia gharama

Na Mwandishi Wetu, Arusha
WIZARA ya Kazi na Ajira imeombwa kuunga mkono na kutetea viwanda vya nguo
vya hapa nchini ili kupunguziwa gharama za uzalishaji, hatua itakayoviwezesha kuzalisha zaidi na kuongeza ajira kwa vijana nchini.
Ombi hilo lilitolewa juzi kwa Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dkt. Makongoro Mahanga, alipotembelea kiwanda cha A to Z cha mjini Arusha, kinachozalisha vyandarua na aina nyingine za nguo.
Mwekezaji na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni A to Z, Bw. Anuj Shah, aliitaka serikali kuangalia mfumo mzima wa kodi kwenye viwanda vya nguo nchini, ili viweze kushindana kwenye soko huru la nguo.
Alisema hiyo ni kwa kuzingatia kuwa sekta ya viwanda vya nguo, ndiyo sekta yenye uwezo mkubwa zaidi wa kutoa ajira kuliko aina zingine za viwanda.  Kiwanda cha A to Z, kimeajiri wafanyakazi 7,500.
Bw. Shah, alimhakikishia Dkt. Mahanga kuwa kama serikali itasikia kilio chao kuangalia mfumo wa kodi kwenye baadhi ya vifaa, malighafi na bidhaa katika kiwanda chake, ana uhakika kufikia mwaka 2015 kiwanda kitakuwa kinaajiri Watanzania 10,000 kama Rais Jakaya Kikwete, alivyowaomba  alipokizindua mwaka 2006.
Hata hivyo Bw. Shah alisema ahadi hiyo itategemea pia mwelekeo wa soko la vyandarua linaloelekea kudorora kutokana na misaada ya vyamdarua vya bure kutoka mashirika kadhaa ya kimataifa kwa mataifa masikini kama Tanzania yanayokabiliwa na malaria.
Akijibu ombi hilo, Dkt. Mahanga alisema serikali italifanyia kazi ombi hilo. Alisema wizara yake lazima iwe karibu na sekta za uzalishaji zenye uwezo wa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.
"Kwa kuwa sekta ya kwenye viwanda, hasa  vya nguo ndiyo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi kutokana na aina ya uzalishaji, ambapo rasilimali watu lazima itumike kwa wingi kwenye mzunguko, ombi lenu serikali italifanyia kazi," alisema Dkt. Mahanga.
Aliongeza kuwa kutokana na uwezo huo mkubwa wa kuzalisha ajira nyingi na ushindani mkubwa kwenye soko ni vema wizara yake ikasikiliza na kuwasaidia wawekezaji kwenye viwanda vya nguo kuhusu kilio chao cha kupunguziwa baadhi ya kodi.
Alimpongeza mwekezaji huyo, si tu kwa kuweza kuajiri Watanzania wengi, lakini pia kujali maslahi ya wafanyakazi ikiwemo mishahara ya kuridhisha, malipo mengine na huduma za usafiri, matibabu na nyumba za wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment