16 January 2012

James Kibosho apata ulaji Twanga

Na Mwandishi Wetu

MPIGA ngoma wa bendi ya muziki wa dansi ya African Stars 'Twanga Pepeta', James Kibosho, amerithi mikoba ya aliyekuwa mwimbaji wa bendi hiyo, Charles Gabriel 'Chaz Baba' aliyetangaza kujiengua wiki hii na kuhamia Mashujaa Musica.

Mmoja wa wanamuziki nguli wa Twanga Pepeta, Khamis Kayumbu 'Amigolas' juzi usiku alimtangaza Kibosho kuwa ndiye kiongozi wa kupanga muziki jukwaani (Stage Master), nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Chaz Baba.

Tangazo hilo la Amigolas, lilipokewa kwa hoi hoi, nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wa Twanga Pepeta waliofika katika Ukumbi wa Maisha Klabu, Dar es Salaam.

Twanga Pepeta hivi sasa inatamba na albamu yake ya 11 ya Dunia Daraja yenye nyimbo za Kauli, Kiapo cha Mapenzi, Umenivika Umasikini, Mtoto wa Mwisho, Dunia Daraja na Penzi la Shemeji.

Albamu zilizopita za bendi hiyo ni Kisa cha Mpemba (1999), Jirani (2000), Fainali Uzeeni (2001), Chuki Binafsi (2002), Ukubwa Jiwe (2003), Mtu Pesa (2004), Safari 2005 (2005), Password (2006), Mtaa wa Kwanza (2007) na Mwana Dar es Salaam (2009).

No comments:

Post a Comment