16 January 2012

Samatta, Ochan ruksa kucheza CAF

Na Zahoro Mlanzi

HATIMAYE mshambuliaji wa timu ya taifa (Taifa Stars) na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samatta amepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) baada ya timu yake kuomba kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Mbali na kukubali kutoa hati hiyo, lakini TFF imetoa sharti la kuitaka timu hiyo ndani ya siku 30 baada ya kupokea ITC, ihakikishe inalipa fedha za kuendeleza mfuko wa timu, ambazo ni asilimia 5 za uhamisho wake kwenda kwa timu ambazo mshambuliaji huyo alipitia.

Akizungumza Dar es Salam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema wamepokea maombi ya ITC ya Samatta, ambayo tayari wameshaituma Congo.

"Tulipokea maombi hayo na pia si Samatta tu, ikumbukwe hata Patrick Ochan naye hakuombewa hivyo wameomba ITC mbili za wachezaji hao na tayari tumeshazituma, hivyo wanaweza kucheza michuano yoyote," alisema Wambura na kuongeza;

"Lakini kwa upande wake Samatta, pamoja na kutolewa kwa ITC yake kama sheria za FIFA vinavyoekekeza katika kifungu cha nne cha utaratibu wa uhamisho, bado TP Mazembe wana deni kwa upande wa timu ambazo mchezaji huyo alipitia," alisema.

Alisema kutokana na hilo wanatakiwa kulipa asilimia tano ya mfuko wa kuendesha timu alizopitia ndani ya siku 30, baada ya kupokea hati ya Samatta, vinginevyo wakishindwa kufanya hivyo kwa wakati watachukua hatua itakayostahili.

Wambura alisema fedha hizo, zitakwenda kwa timu ya Kimbangulile na Mbagala Market ambayo sasa ni African Lyon ambapo fedha hizo zitagawanywa kulingana na jinsi sheria inavyoelekeza.

Samatta alijiunga na timu hiyo akitokea Simba kwa uhamisho wa zaidi ya sh. milioni 180 pamoja na Ochan, lakini kwa ada tofauti za uhamisho ambapo uhamisho huo uliweka rekodi nchini.

No comments:

Post a Comment