16 January 2012

Botswana yatishia 'nyau' vigogo CAN 2012

GABORONE,Botswana

TIMU ya Taifa ya Botswana, imesema  itafanya maajabu makubwa kwenye fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika  kuanzia mwishoni mwa wiki hii katika nchi za Guinea ya Ikweta na Gabon, huku ikizitahadharisha timu zitakazokutana nazo kukaza buti.

Timu hiyo iliwashangaza wengi baada ya kutinga fainali hizo kwa kuzipiku timu zilizokuwa zimepangwa kundi la tano ambalo lilikuwa na timu za  Tunisia, Togo, Malawi na  Chad.

Kutokana na hali hiyo ndiyo maana ikatunukiwa tuzo ya timu bora ya mwaka jana kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mbele ya vinara wa soka Ivory Coast, Tunisia na  Niger.

"Nina furaha kubwa kwa mara ya kwanza kufuzu fainali za mashindano haya na kutwaa tuzo hii," alisema kocha wa timu hiyo Stanley Tshosane na kuongeza;

 "Ni mafanikio makubwa ambayo yanatusukuma kufanya kazi kubwa kutokana na kwamba watu wengi kwa sasa wanatarajia mengi kutoka kwetu,"alisema na kusisitiza kwamba hatua hiyo ni jitihada binafsi za timu na hivyo wanaitunuku tuzo hiyo.

Tshosane ameinoa timu hiyo ndani ya  miaka mitatu lakini inamlazimu kusubiri hadi zimalaizike fainali hizo ili aweze kupewa mkataba mpya.

Katika fainali hizo,Pundamilia hao wamepangwa Kundi D ambapo Januari 24  itakutana na Ghana mjini Franceville, Gabon.

Inaelezwa kuwa timu hiyo itakuwa ni moja ya timu zilizojiandaa vyema katika fainali hizo, baada ya kuweka kambi kwa muda mrefu katika nchi za Afrika Kusini, Falme za Kiarabu na  Cameroon.

Mbali na kuweka kambi kwa mujibu wa Shirika la Habari la Marekani (AP), timu hiyo pia imecheza mechi nyingi za kujipima nguvu zikiwamo ambazo ilitoka suluhu na Nigeria na ile ambayo matokeo ni 1-1 dhidi ya Namibia kabla ya kwenda tena suluhu na Zimbabwe ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani.

No comments:

Post a Comment