28 December 2011

Yanga sasa wamkumbuka Mosha

*Wapanga kuandama kumrejesha

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya wanachama wa Yanga, wameanza harakati za kumtafuta Makamu Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo Davis Mosha, arejee na ili kuokoa jahazi
kutokana na kukabiliwa na ukata.

Juzi Kocha Mkuu wa timu hiyo Kostadin Papic, alizungumzia hali ngumu ya maisha kwenye klabu hiyo, akihitaji wenye mapenzi na Yanga wajitokeze kuisaidia timu hiyo, inayokabiliwa na njaa ya kutisha.

Baadhi ya wanachama Yanga jana waliamua kukutana Dar es Salaam kuangalia mustakabali wa timu hiyo, huku wengine wakipiga mahesabu jinsi ya kushawishi Mosha arejee tena katika klabu hiyo kongwe nchini.

Hata hivyo wakati wanachama hao wakihaha kuinusuru timu yao Mosha mwenyewe kwa sasa yupo Moshi katika sikukuu za Krismasi.

Wanachama hao waliamua kutaka kuushiniki uongozi kuitisha Mkutano Mkuu, ili kutumia nafasi ya kumrudisha Mosha kundini.

Akizungumzia suala hilo Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Tawi la Yanga la Chalinze, Adam Kiponzile mwenye kadi namba (006180) alisema kwamba kuna haja ya Mosha kurudishwa haraka iwezekanavyo, ili ainusuru timu yao.

Alisema hali ndani ya Yanga imekuwa tete, hivyo Mosha lazima arudishwe tena kwa heshima ili kuokoa ugumu wa maisha unaoendelea ndani ya timu yao.

“Sitaki kuona ugumu huo unaendelea kuwa tatizo kwa wachezaji wetu, maana tunaamini Mosha ni mchapakazi na mwenye moyo wa dhati wa kuongoza Yanga kwa mapenzi makubwa kwa siku nyingi.

“Angalia hadi kocha analalamikia maisha magumu, lakini viongozi hawana jipya na wanatudanganya kujipanga vyema kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi, wakati hakuna maandalizi yoyote kutokana na ukata,” alisema Kiponzile.

Kwa mujibu wa Kiponzile, wanachama wote wenye mapenzi mema na klabu hiyo, wapo tayari kuandaa maandamano ya nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo aweze kurejea ndani ya Yanga ili alete maendeleo.

Naye mwanachama mwingine wa Yanga, Juma Msanga mwenye kadi namba (10650) alisema ugumu wa maisha ndani ya Yanga, utakwisha endapo Mosha atakubali kurudi awe kiongozi au mdhamini wa klabu.

“Huu si wakati wa viongozi wetu kuendelea kubaki kimya, wakati wanajua hawana uwezo wa kufanya lolote la maana, hali inayokera watu akiwamo kocha Papic, aliyeshindwa kuvumilia njaa,” alisema Msanga.

Gazeti hili lilifanya uchunguzi katika matawi kadhaa ya jijini Dar es Salaam na kukutana mijadala kila mmoja akisema lake, huku wengi wao wakionesha chuki baada ya kauli ya Papic.

No comments:

Post a Comment