*Wasababisha kero kubwa, wananchi walalamika
BAADHI ya wamiliki wa vituo vya mafuta Jijini Dar es Salaam, jana walifanya mgomo baridi wa kutouza mafuta ya petroli katika vituo vyao ili kupinga
bei elekezi iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Uchunguzi uliofanywa jana katika vituo mbalimbali vya mafuta, umebaini baadhi ya vituo vilisitisha kuuza bidhaa hiyo kwa madai nishati hiyo imekwisha.
Mmiliki wa kituo kimoja cha mafuta ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema baadhi ya vituo vilifanya mgomo baridi wa kuuza mafuta ili kushinikiza bei ya bidhaa hiyo ipandishwe.
“Wenzetu wapo katika mgomo lakini sisi tunauza kama kawaida, sijui kesho (leo) pengine kutakuwa na mabadiliko, lakini ukweli ni kwamba baadhi ya vituo vipo katika mgomo baridi,” alisema.
Wakati mgomo huo ukilaaniwa na wananchi mbalimbali ambao jana walipata shida kubwa ya usafiri, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati ya Maji (EWURA), imekanusha madai ya kuwepo kwa mgomo huo.
Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Mamlaka hiyo, Bw.Titus Kaguo, alisema hakuna mgomo wowote unaoendelea katika vituo vya kuuzia mafuta.
Alisema mabadiliko ya bei ni makubwa hivyo kwa mtu yeyote ambaye ana mtaji mdogo lazima atakufa kibiashara.
“Mtu mwenye mtaji mdogo itambidi aagize mafuta kuanzia Jumatatu ili asubiri kama kutatokea mabadiliko mapya,” alisema.
Aliongeza kuwa, katika punguzo kama hilo mfanyabiashara anakuwa makini ili asije kupata hasara kwani biashara hiyo haina tofauti na nyingine ambayo inaweza kuleta faida na hasara.
Hata hivyo alisema kwa mujibu wa ripoti aliyonayo, mafuta ya petroli na dizeli yapo ya kutosha na kushauri wananchi waende kununua mafuta hayo katika vituo vya Gapco na Oil Com.
Waandishi wa gazeti hili walitembelea baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta na kukuta vituo hivyo vimefungwa na vingine vikiwa vimesitisha huduma hiyo na kudai mafuta ya petroli yamekwisha.
Hata hivyo vituo vingine vilikuwa vinatoa huduma ya mafuta ya taa na dizeli kwa kuwa mafuta hayo bado haijashuka bei.
Majira lilishuhudia baadhi ya wafanyakazi wa vituo hivyo wakisema hawawezi kuuza petroli kwa bei ya hasara wakati bei waliyonunulia ni kubwa.
“Hatuwezi kuuza petroli kwa bei ya hasara, ni bora kuwaambia wateja hakuna mafuta,” walisema wauzaji hao.
No comments:
Post a Comment