20 December 2011

Tendwa amlilia Kafulila

*Ataka busara itumike kumaliza mgogoro uliojitokeza
*Asema ipo hatari ya chama hicho kupoteza umaarufu
*Nape: Mimi si mfuasi wa siasa za kufukuza vijana
*Aishukuru NCCR kurudisha jimbo hilo kwa CCM


Agnes Mwaijega na Paulina Lyapa

MSAJILI wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa, amesema hajafurahishwa na uamuzi wa Chama cha NCCR-Mageuzi, kumvua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini, kwa tiketi ya
chama hicho Bw.David Kafulila.

Alisema kitendo hicho ni fedheha kwa chama hicho ambacho kinaweza kupoteza mvuto na umaarufu wake mbele ya jamii hata kukibomoa.

Bw.Tendwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mada katika semina ya viongozi wa Baraza la Vyama vya Siasa nchini.

“NCCR-Mageuzi inapaswa kutumia busara kubwa kuhakikisha suala hili linatatuliwa kwa njia ya demokrasia ambayo itajenga taswira nzuri kwa jamii,” alisema Bw.Tendwa.

Alisema chama hicho kinapaswa kutumia njia mbadala ya kumwajibisha Bw.Kafulila kwa kufanya vikao vya ndani badala ya kumfukuza kama walivyofanya.

“Kimsingi kuna adhabu nyingi ambazo zingeweza kutumika ili kumkanya mbunge au mwanachama wa chama chochote cha siasa lakini siwezi kuingilia maamuzi ya NCCR-Mageuzi kwa sababu huo ni utaratibu wao,” alisema.

Akisisitiza msingi wa hoja yake, Bw.Tendwa alisema suala hilo halikupaswa kufikia hatua nzito kama hiyo ambayo taifa litatumia fedha nyingi kufanya uchaguzi mdogo.

“Kwa mujibu wa sheria na taratibu, mbunge akivuliwa uanachama na chama chake, anapoteza ubunge na nafasi nyingine za siasa anazozitumikia,” alisema.

Aliwataka viongozi wa vyama vyote vya siasa nchini kuwa makini na maamuzi yao kwa manufaa ya taifa.

Wiki iliyopita, Bw.Kafulila na wenzake walifukuzwa uanachama katika kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu NEC ya chama hicho, kilichofanyika jijini Dar es Salaam kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuzungumzia masuala ya chama nje ya utaratibu.

Akizungumza na Majira juzi, Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Bw.Freeman Mbowe, aliweka wazi kuwa bado anaamini NCCR-Mageuzi wanaweza kutumia busara kumaliza suala hilo badala ya kuliingiza taifa katika uchaguzi mdogo ambao utatumia fedha nyingi za walipa kodi.

Awali akitoa mada katika semina hiyo kuhusu misingi ya uongozi, Bw.Tendwa alisema vyama vyote vya siasa vinatakiwa kuwa na utaratibu wa kuainisha mfumo wa mamlaka na majukumu katika miundo ya vyama vyao.

Alisema hatua hiyo itapunguza migongano inayotokana na udhaifu katika kuainisha ukomo wa madaraka ya mamlaka husika na kuongeza kuwa migawanyiko ndani ya chama siyo mizuri kwani inaweza kusababisha chama husika kishindwe kufikia malengo yake.

“Upo umuhimu wa kila chama kuhakikisha kinawajengea uwezo viongozi wa chini ili waweze kurithi misingi ya uongozi kwani hakuna kiongozi anayeweza kuongoza milele, mnapaswa kuwapa changamoto wengine ili wajiamini,” alisema.

Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa semina hiyo Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa NEC ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw.Nape Nnauye, alisifu ofisi ya Bw.Tendwa kuandaa mafunzo hayo ambayo ni muhimu kwa masilahi ya taifa.

Alisema suala la maadili kwa viongozi wa siasa ni muhimu na kama yatakosekana, athari zake kwa taifa ni kubwa.


Bw.Nnauye amelaani kitendo cha NCCR-Mageuzi, kumfukuza Bw.Kafulila na kudai kuwa kitendo hicho hakilengi kuwajenga vijana kuwa wanasiasa wazuri badala yake kinawakatisha tamaa kuingia katika siasa na kuwapoteza.

Alisema chama hicho kinapaswa kutumia njia nyingine ya kumuadhibu kama alifanya kosa badala ya kumfukuza uanachama.

“Mimi si muumini wa siasa za kuwafukuza wanasiasa vijana katika vyama, tukiendeleza utamaduni huu wa kufukuza vijana kila wanapokosea badala ya kuwarekebisha, tutawakosa katika siasa.

“Naamini katika siasa uvumilivu unahitajika pamoja na kuwafundisha vijana badala ya kuwafukuza, binafsi sitaki kuingilia uamuzi wa NCCR-Mageuzi, lakini kama mwanasiasa kijana, naamini kuwafukuza vijana kila wanapokosea si njia sahihi ya kuwarithisha uongozi wa vyama hivyo na taifa kwa ujumla,” alisema.

Aliongeza kuwa, uchaguzi mdogo unaigharimu nchi fedha nyingi ambazo zingetumika katika shughuli nyingine za maendeleo.

Alipoulizwa maoni yake kuhusu uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kigoma Kusini kama maamuzi dhidi ya Bw.Kafulila yatabaki kama ilivyoamuliwa alisema, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaishukuru NCCR kuwarudishia jimbo hilo kutoka mikononi mwa upinzani.

“Nawashukuru NCCR-Mageuzi kwa uamuzi wao wa kuamua kuturudishia Jimbo la Kigoma Kusini kilaini, kama uchaguzi mdogo ukifanyika tutashinda,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za tathmini ya hali ya kisiasa nchini, hakuna uchaguzi mdogo ambao CCM itashindwa ambapo jambo hilo liko wazi.

Kuhusu uwezekano wa Bw.Kafulila kukata rufaa, alisema hana imani kama jambo hilo linaweza kubadilika kwani aliyesimamia maamuzi ya kufukuzwa kwake, ndiye Mwenyekiti wa kikao cha rufaa.

Alipoulizwa kama CCM inaweza kumpokea Bw.Kafulila kama ataamua kujiunga na chama hicho alisema milango ipo wazi.

“Hata akijiunga na chama chetu, siwezi kusema anaweza kuteuliwa kuwa mgombea, CCM inataratibu zake,” alisema.

10 comments:

  1. UKIMUONA MCHAGA KANG'ANG'ANIA MAHALI UJE KUNA PESA. HIVYO VYAMA VYENYE WACHAGA VIONGOZI NI KAMPUNI ZAO BINAFSI ZA KUTAFUNA PESA ZA WANANCHI. BORA HIYO CCM KULIKO HAO WACHAGA WAKISHIKA NCHI WATANZANIA MMEKWISHA.

    ReplyDelete
  2. mpumbavu kabisa uliyeandika hapo juu! ulimwengu huu si zama za ukabila! Nahisi hata shule hujaenda!

    ReplyDelete
  3. Gharama za uchaguzi mdogo ni kubwa, lakini gharama ya demokrasia ni kubwa zaidi.Huwezi kukwepa gharama kwenye kutafuta haki na demokrasia.Vijana wanajifunza/ wanafundishwa kwa njia nyingi, hata kuwavua uanachama ni somo kwa wengine, kwani, demokrasia pia ina mipaka na miiko yake,upo hapo kijana wa kujivua gamba!

    ReplyDelete
  4. Tendwa ana machozi mengi ya bure. Je anamlilia Kafulia au ni machozi ya mamba? Muache Kafulia ajililie mwenyewe kwa kunywa alilokoroga mwenyewe. Tamaa mwisho wake huwa hivyo. Hakuna cha kuliliana hapa bali kupeana ukweli.
    Mpayukaji

    ReplyDelete
  5. WACHAGA SIKU ZOTE NI TATIZO, WAKIPATA MADARAKA HUWA HAWATAKI KUYAACHIA, SIO KWA KAFULILA NA MBATIA HATA ZITO KABWE KWA MBOWE, ALIPOONA ANAKARIBIA KUSHINDWA ZILIPITA FITINA NYINGI MPAKA KUMTOA ZITO KWENYE KINYANG'ANYIRO, WASHINDWE WACHAGA NA UONGOZI WA JUU WA NCHI HIII

    ReplyDelete
  6. Kweli we mwenyewe siunaona CHADEMA nafasi zote za kwao, angalia viti maalum, wamejazana wenyewe tu kwani chama ni cha ukoo, acheni bwana chama sio kiamba ebo!!

    ReplyDelete
  7. ni kweli ukabila ni mwingi sana tanzania angalia hata ajira vyuoni UDOM wamejaa watu wa mikoa ya kusini(iringa,mbeya na songea) na kwenye vyombo vya habari IPP wamejaa wachaga watupu.zinatolewa kwa kuangalia nani anatoka wapi.. kwenye siasa wanaopewa nafasi ni wale wanaojulikana au kuwa na uhusiano na viongozi wao.. angalia ngazi za juu CHADEMA, TLP na NCCR.. hata nafasi za viti maalumu zilitolewa kwa ukabila na udini.

    ReplyDelete
  8. naamini wote mliopita hapo juu isipokuwa mmoja wenu ana macho yenye akili kwani nikionacho hapo ni anti CHADEMA. KWAHIYO MARANDO NA SLAA NI WACHAGA? PROF SAFARI NAE MCHAGA NA MNYIKA JE? MSIWE MBUMBUMBU WA KUIGA MANENO YA VIONGOZI WA MAGAMBA KAMA KASUKU. MSYANI HAPA.

    ReplyDelete
  9. PENYE UKWELI UONGO HUWA HUJITENGA... SLAA SIO MCHAGA ILA ANATOKA KULE KULE KASKAZINI! NA HIVI HAKUNA WASUKUMA, WADIGO, WAMAKONDE CHADEMA??? HIKI SIO CHAMA NI TAASISI YA NDESAMBURO NA UKOO WAKE KUJINUFAIFA KAMA ILIVYO NCCR!

    ReplyDelete
  10. ACHA UBWEGE CHADEMA NI KOMBAIN YA TZ MBONA WASUKUMA WAKURYA WAHAYA WAKINGA WAARABU WANA VYEO CHADEMA.ACHENI UNAFIKI

    ReplyDelete