02 December 2011

Watoto zaidi ya 300 watoroshwa kuchanjwa Dodoma

Na Bryceson Mathias

WATOTO 349 kati ya 350 wenye umri chini ya miaka mitano wanaotakiwa kupatiwa chanjo ya kinga ya polio,surua na vitamin A katika
Kijiji cha Ntyuka Wilaya ya Dodoma Mjini, wametoroshwa na wazazi wao ili wasipatiwe huduma hiyo kwa madai ya kupigiwa simu na ndugu zao kutoka maeneo mengine kuwa wanaochanjwa wanakufa.

Tukio hilo la aina yake ilitokea juzi Novemba 29 saa saba mchana wakati watoto hao walipokuwa wakiandaliwa kupata chakula kabla ya chanjo na ghafla wazazi walitokea kila pembe ya Kijiji hicho na kuanza kuwachukua watoto wao na kuwatorosha.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ntyuka Bw. Wilson Chimbwi, alithibisha tukio hilo huku akionyesha hali ya masikito.

“Nimesikitishwa na wananchi wa kijiji changu kuwatorosha watoto 349 wasichanjwe, ni mtoto mmoja tu ndiye aliyepatiwa chanjo mzazi wake ni Bi. Eva Meshack (5), wazazi hao walidai kuwa watoto wanne waliochanjwa Kikuyu walikufa, hata hivyo taarifa hizo za kufa kwa watoto waliochanjwa si za kweli,” alisema bw. Chimbwi. 

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na hali hiyo walilazimika kusitisha shughuli hiyo kijijini kwake baada ya watoto karibu wote kutoroshwa na wazazi hivyo wahudumu waliopewa mafunzo Kaloleni Dodoma kwa ajili ya kutoa chanjo kubaki wakiwa hawana cha kufanya.

Mmoja wa Walimu wa shule ya awali ambaye pia alipewa mafunzo ya kutoa chanjo Bi. Mariam Daniel (37), alikiri watoto hao kutoroshwa mara tu baada ya kumpatia chaanjo mtoto wa Bi. Meshack na kwamba wazazi walitokomea na watoto wakati wakiandaliwa.

Mmoja wa wazazi Bi. Ester John (27) alisema, “Nilichukua wanangu na wadogo zangu wasichanjwe baada ya kupigiwa simu na ndugu zetu walioko Kikuyu kwamba kuna watoto wanne Nkuhungu ambao wamefariki baada ya chanjo,".

Hata hivyo Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Godfrey Mtei, alipinga taarifa hizo za watoto kupoteza maisha baada ya kuchanjwa na kuongeza kuwa hizo ni uzushi.

Mmoja wa wazazi jina tunalo alidaiwa kuwashawishi wazazi wenzake kutokubali watoto wao kuchanjwa akisisitiza madai ya kuwepo kwa vifo kwa waliopatiwa huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment