Na Mnaku Mbani
KATIKA hali inayoonyesha kuongezeka kwa ukata katika masoko ya fedha nchini, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeshindwa kukusanya sh. bilioni 20. Kiasi hicho kilitarajia
kukusanywa jana kupitia uuzwaji wa amana za serikali (Treasury bonds) za kipindi cha miaka kumi.
Kwa mujibu wa ripoti ya mauzo ya amana hizo, sh.milioni 926 tu ndizo zilizopatikana fedha ambazo ni chini ya asilimia 50 ya kiwango kilichopangwa kukusanywa.
Fedha hizo kwa mujibu wa taarifa za awali zilipangwa kukusanywa ili kugharamia bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha 2011/2012.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha mwisho wa mwaka kwa serikali kushindwa kukusanya fedha kupitia amana zake.
Siku chache zilizopita serikali ilishindwa kukusanya sh. bilioni 100 kutoka katika soko hilo badala yake ikakusanya sh. bilioni 13.56 tu.
Hali hii inatokea wakati BoT tayari ilishapandisha viwango vya riba kwa mwezi Novemba viwango ambavyo vimetabiriwa na wataalamu wa uchumi kuwa vitaathiri mikopo ya sekta binafsi.
Bw.Joel Nkya, mchambuzi wa masuala ya masoko ya fedha wa kampuni ya Tanzania Securities Limited, alisema anaamini hali hiyo inatokana na ukosefu wa fedha katika soko.
"Hali hii inasababishwa na ukosefu wa fedha hasa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka ambapo benki nyingi hazifanyi biashara kutokana na kufunga mahesabu ya mwaka," alisema Bw.Nkya katika mahojiano kwa njia ya simu.
Hata hivyo Nkya alisema bado suala la riba ndogo kwa amana za muda mrefu ikilinganishwa na zile za muda mfupi linawavunja moyo wawekezaji wengi wa masoko ya fedha.
Alisema wawekezaji wengi wa masoko ya fedha huenda wakapeleka fedha zao benki kwa kuwa taasisi hizo zimepandisha riba kwa wateja wa akiba za muda mrefu.
Aliishauri serikali kupitia upya viwango vya riba za amana za muda mrefu ili kuvutia wawekezaji iwapo inapenda kufanikiwa katika ukusanyaji wa fedha za kutosha.
Hivi karibuni ilitolewa tangazo kwamba katika mwaka wa fedha 2011/2012 ulioanza mwezi Julai mwaka huu serikali inakabiliwa na upungufu wa kiasi cha sh. bilioni 780 kutokana na kupanda kwa mfumuko wa bei.
Pengo hilo lilitarajiwa kuzibwa kwa serikali kukusanya kodi na pia ilipanga kuuza amana zake za muda mfupi na mrefu.
Ripoti za BoT zinaonyesha kwamba tayari serikali imeshakopa sh.trilioni 1.06 kwa kuuza amana zake katika kipindi cha nusu ya mwaka 2011/2012 unaoishia mwezi huu, kiwango ambacho ni kikubwa ikilinganishwa na malengo yake.
Katika bajeti ya mwaka 2011/2012 serikali ilipanga kukusanya sh.trilioni 1.2 kwa kuuza amana zake lakini hivi karibuni, Waziri wa Fedha, Bw. Mustafa Mkulo, alitangaza kuwa tayari serikali imekopa sh. trilioni moja kutokana na uuzaji wa amana za muda mrefu na mfupi.
Wadadisi wa masuala ya uchumi wameonya kwamba iwapo serikali itaendelea na kukopa katika mifumo ya ndani ya fedha zikiwemo benki za biashara, itasababisha kudorora kwa utoaji mikopo kwa sekta binafsi kwa kuwa wawekezaji wengi hukimbilia amana kwa sababu ulipwaji wake ni wa uhakika.
Katika kipindi cha mwaka huu wa fedha serikali inatarajia kukusanya sh.trilioni 6.2 huku matumizi yakifikia trilioni 11.
No comments:
Post a Comment