29 December 2011

TRA kurejesha VAT kwa wageni

Na Zena Mohamed

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza utaratibu wa kuanza kurejesha Kodi ya Ongezeko la Thamani VAT iliyolipwa na raia wa kigeni punde watakapoondoka na
bidhaa hizo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Fedha wa TRA, Bw. Saleh Mshoro, alisema utaratibu huo utaanza Januari mosi mwakani na kwamba ni mfumo unaotumika sehemu mbalimbali duniani.

Alisema anayestahili kurejeshewa VAT ni msafiri yeyote ambaye si raia wa Tanzania anayesafiri kwenda nje ya nchi akiwa na bidhaa aliyoinunua kwa rejareja na kuilipia kodi hiyo.

Bw.Saleh alisema kwa kawaida VAT hutozwa kwa bidhaa mpya hivyo iwapo raia wa kigeni wanaondoka na bidhaa hizo si vema kutozwa kodi hiyo nchini.

Alisema mpango huo unalengo la kukuza biashara za nje na ili kuufanikisha serikali kupitia Bunge la bajeti mwaka huu ilifanya marekebisho ya sheria ya VAT na kuridhia kuanza kwa utaratibu wa kurejesha VAT iliyolipwa na raia wa kigeni wanaoondoka nchini wakiwa na bidhaa kwa matumizi ya nje ya nchi.

Alitaja masharti yatakayotumiwa kufanikisha utaratibu huo kuwa ni mwombaji kuwa na stakabadhi inayoonesha maelezo ya bidhaa aliyonunua na kutolewa na mashine za kielektroniki (EFDs).

Alisema utaratibu huo utathibitisha madai ya mwombaji ili kurejeshewa VAT iliyolipwa na kwamba marejesho yatafanyika katika viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Julius Nyerere na Kilimanjaro (KIA).

Masharti mengine ni marejesho kutolewa kabla ya miezi sita tangu stakabadhi ilipotolewa, thamani ya bidhaa zinazostahili marejesho kutokuwa chini ya sh.400,000 za kitanzania, bidhaa zilizonunuliwa kutotumika na msafiri kuwa na hati ya kusafiria, tiketi na hati ya kuruhusiwa kupanda ndege.

"Naliwaomba wote wanaostahili kudai marejesho pamoja na umma kwa ujumla kushirikiana nasi kutoa huduma bora na yenye ufanisi wa hali ya juu kwa kuzingatia sheria zinazo husika,"alisema.

1 comment:

  1. Hivi ina maana sheria hii ya kuwarudishia VAT raia wa kigeni ni pale wanaposafiri kwa ndege tu? Wanaposafiri kwa barabara hawastahili hayo marejesho? Kama ndivyo, mantiki yake nini? Suala lingine, kwa nini raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi nao wasirudishiwe hiyo VAT ikiwa nao wanaenda kutumia hizo bidhaa nje ya nchi?

    ReplyDelete