21 December 2011

Mwambungu aipiga jeki Majimaji

Na Mhaiki Andrew, Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ametoa msaada wa mipira 11 yenye thamani ya sh. 660,000 kwa Klabu ya Majimaji ili iweze kufanya vizuri katika
mashindano ya Ligi ya Taifa ya Daraja la kwanza.

Akizungumza mjini hapa juzi kabla ya kukabidhi mipira hiyo, Mwambungu alisema Majimaji inahistoria ndefu kwenye Mkoa wa Ruvuma, ikilinganishwa na timu nyingine katika kulitangaza jina la mkoa ndani na nje ya nchi.

Alisema msaada huo, ataendelea kuchangia kwa kuwashawishi wakazi wa ndani na nje ya mkoa, ili kuisaidia timu hiyo iweze kufanya vizuri katika awamu ya pili ya ligi hiyo, ambayo itaanza Januari mwakani.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema msaada huo wa mipira, utakuwa chachu kwa wachezaji wao kujituma kufanya mazoezi kwa nguvu.

Pia aliwataka viongozi wa klabu hiyo, wawe waaminifu na waachane na tamaa ya kutaka kunufaika kupitia misaada inayotolewa na wahisani, kwani kufanya hivyo watakuwa wameua maendeleo ya klabu yao na mkoa kwa ujumla.

Alisema pamoja na kuipatia msaada wa mipira 11, pia aliahaidi kuisaidia timu ya Mlale JKT inayoshiriki ligi hiyo ya Daraja la kwanza na Shule zote za Sekondari za Mkoa wa Ruvuma kwa kuwapa mipira miwili kila shule ili ziweze kuwapika wachezaji na kuibua vipaji kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma.

No comments:

Post a Comment