21 December 2011

SUMATRA yakana kupanda nauli mabasi ya mikoani

Na Anneth Kagenda

WAKATI wananchi wakiilalamikia serikali kuhusu kupanda ghafla kwa nauli za mikoani katika kipindi hiki cha sikukuu ya Krismasi, Mamlaka ya Usafirishaji wa Majini na
Nchi Kavu (SUMATRA) imepinga kuwepo kwa kero hiyo na kudai kuwa ni uzushi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu jana, Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki, Bw.Conlad Shio, alisema wahusika wa mabasi ya mikoani wanatoza bei halali zilizopangwa na mamlaka hiyo.

Alisema si kweli kwamba kuna watu wanatoza bei ya juu kwa kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamejipanga vizuri kukabiliana na wote watakaojaribu kufanya hivyo.

Licha ya kupinga kuwepo kwa kero hiyo, pia Bw.Shio alikiri kwamba abiria wawili wa kiume na wa kike walilanguliwa kwa kutozwa sh.35,000 kwa safari ya Dar es Salaam - Kilimanjaro badala ya bei halisi ya sh.24,500 au 16,400.

"Tulipoingia kwenye gari hilo linalofanya safari zake Dar - Moshi na kuuliza kama kuna mtu kalanguliwa kwa kuuziwa tiketi kinyume na maagizo ya SUMATRA watu hao wawili walijitokeza

"Baada ya kuwauliza walituambia walikatiwa tiketi hizo na vijana waliokuwa nazo mkononi pasipo kujua kwamba kufanya hivyo ni kosa," alisema Bw.Shio.

Aliwataka wamiliki wa mabasi kutoa maelezo kwa wasimamizi wa vyombo hivyo pamoja na makarani wao na kuonya kuwa wasipofanya hivyo SUMATRA itawachukulia hatua kali za kisheria.

"SUMATRA pamoja na polisi hatutakubaliana na ubadhirifu wa aina yoyote kuwalangua abiria fedha za nauli," alisema Bw.Shio.

Awali abiria mbalimbali waliozungumza na gazeti hili waliilalamikia serikali kushindwa kuchukua hatua kudhibiti upandaji holela wa nauli za mikoani katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo.

Walisema licha ya wao kuingia ndani ya kituo hicho na kufika hadi kwenye milango ya mabasi husika wauza tiketi waliovalia sare au nembo za mabasi hayo wamekuwa wakiwauzia tiketi kwa bei tofauti na iliyopangwa na SUMATRA.

Uchunguzi wa Majira katika kituo hicho ulibaini njia inayotumiwa na walanguzi hao kuwa ni kuwajibu abiria kuwa basi limejaa kisha baadaye anakuja mtu mwingine akiwa na tiketi mkononi na kuuza kwa bei ya juu tofauti na ilivyopangwa.



No comments:

Post a Comment