21 December 2011

Kibanda kizimbani kwa madai ya uchochezi

Na Rehema Mohamed

MHARIRI Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Bw.Absalom Kibanda na mwenzake wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la
kuhamasisha kutotii mamlaka halali ya nchi (Uchochezi).

Mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Mhasibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bw.Samson Mwigamba, ambaye hakuwepo mahakamani hapo jana wakati shtaka hilo likisomwa.

Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa kwenye kesi nyingine inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Mbele ya Hakimu Bw.Stuwart Sanga, wakili wa serikali, Bi.Elizabeth Kaganda, alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa hilo Novemba 30, mwaka huu.

Alidai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kupitia makala iliyokuwa na kichwa cha habari 'Waraka maalumu kwa askari wote' iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima toleo namba 2553 la mwaka huu.

Mshtakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo wakili wa serikali, Bi.Kaganda alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo Bw.Kibanda yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini hundi ya sh.milioni tano kila mmoja pamoja na mdhamini mmoja kati ya hao  kuwasilisha mahakamani hapo hati ya nyumba.

Bw.Kibanda pia aliamriwa kuwasilisha mahakamani hapo hati ya kusafiria pamoja na kupewa sharti la kuripoti Polisi Makao Makuu kila mwezi.

Wadhamini waliomdhamini Bw.Kibanda ni Bw.Said Kubenea, ambaye ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanahalisi na Bw. Aobokile Mwajika, ambaye ni mfanyakazi wa Benki ya Posta.

Katika kesi hiyo Bw.Kibanda anawakilishwa na wakili, Bw.Juventus Mboyi, Bw.Nyaronyo Kichele, Bw.John Mhozya, Bw.Deogratus Ringia na Bw.Isaya Mambo.

Bw.Kibanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) amehojiwa siku mbili Makao Makuu ya Polisi kabla ya kufikishwa mahakamani hapo jana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 19, mwaka huu.



1 comment:

  1. KUMBE GAZETI LA MWANANCHI NA TANZANIA DAIMA LAO MOJA,WANACHAMA WA CHADEMA NDIO WAHARIRI NA WENGINE NI WAKURUGENZI. HIVYO WATANZANIA TUCHUNGE SANA HABARI ZA UPOTOSHAJI ZINAZOANDIKWA NA GAZETI HILI KUFAGILIA CHADEMA KUINGIA MADARAKANI ILI WALE KUKU KWA MRIJA BAADAE

    ReplyDelete