01 December 2011

Redondo apelekwa Moro kwa lazima

Na Zahoro Mlanzi

SIKU chache baada ya kiungo Ramadhani Chombo 'Redondo', kudaiwa kugoma kuichezea timu ya Moro United kwa mkopo, Klabu yake ya Azam FC imesisitiza kwamba atake asitake lazima ataichezea timu hiyo kwa mkopo.

Redondo ni miongoni mwa wachezaji waliotolewa kwa mkopo na timu hiyo akiwemo pia Jamal Mnyate, ambaye pia amepelekwa timu hiyo pamoja na wengine zaidi ya sita wapo Africna Lyon.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa klabu hiyo Jaffar Idd alisema Redondo, bado ni mchezaji wao ila wamempeleka Moro ili akapate nafasi ya kucheza mechi zaidi zitakazomfanya kiwango chake kiimarike.

“Inawezekana dhana ya mchezaji kutolewa kwa mkopo haijaeleweka, tumemtoa kwa mkopo ili kumpa nafasi zaidi ya kucheza kuliko kumwacha hapa, alafu akacheza mara moja moja,” alisema Idd.

Alisema kwa sasa ni mchezaji wa timu ya taifa (Taifa Stars) na ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), hivyo tuna imani kama atacheza mara kwa mara, huko anapokwenda tuna ataendelea kulitumikia taifa kila timu itakapotajwa.

Mbali na kuwatoa wachezaji hao, tayari wachezaji wao wapya Kabolou Tchetche, Gaudance Mwaikimba, Joseph Owino na Abdi Kassim 'Babi' ambao wamesajiliwa wakati wa dirisha dogo, tayari wameshajiunga na wenzao na kuanza mazoezi.

Azam inaendelea na mazoezi katika Uwanja wa Chamazi, uliopo nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam ikijiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, ambao unatarajiwa kuanza Januari, mwakani.

No comments:

Post a Comment