01 December 2011

Jivunie uTanzania yafikia tamati

Na Mwandishi Maalumu

KAMPENI ya Kili Jivunie uTanzania, iliyokuwa ikiendeshwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager, hatimaye imefikia kilele chake baada ya bendera ya taifa kupandishwa katika kilele cha Mlima Kilimanjaro wiki iliyopita.

Bendera hiyo ilipandishwa Jumapili ya Novemba 27 na vijana watatu mahiri, ambao ni watalamu katika masuala ya upandaji milima na uongozaji wa watalii, ambao walitumia saa 20 kupanda mlima huo na kushuka.

Vijana waliopandisha bendera hiyo ni Daniel Ngowi, Revocatus Ngowi na Aloyce Joseph ambao ni maarufu kwa upandaji wa mlima huo na pia uongozaji wa watalii.

Bendera hiyo ilipandishwa baada ya kumalizika kwa mbio za bendera zenye rangi nne za bendera ya taifa, kutoka mikoa minne na baadaye kuunganishwa Moshi na kupatikana bendera moja iliyopandishwa Mlima Kilimanjaro.

Akiwapokea vijana hao juzi katika geti la Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, Wilayani Marangu, Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe aliwapongeza kwa kutimiza malengo ya kampeni ya Jivunie uTanzania.

“Nawapongeza mno kwa kuonesha ushujaa na pia kuandika historia, kwani miaka 50 ya Uhuru haitajirudia tena ni jambo la kujivunia mno,” alisema.

Akizungumza mara baada ya kushuka, Daniel Ngowi alisema: “Najiskia fahari kufanya kitendo hiki cha historia, ambacho sikuwahi kufikiri ningefanya maishani.”

Naye Revocatus Ngowi, alisema kitendo kilichofanywa na Kampuni ya Bia Tanzania kupitia Kilimanjaro Premium Lager cha kupandisha bendera ya taifa katika Mlima Kilimanjaro ni cha historia ya kipekee na kuwa yeye alifarajika kupata fursa ya kupandisha bendera hiyo.

 Naye Aloyce alisema: “Tumechukua saa 20 kupandisha bendera hii katika Mlima Kilimanjaro, pamoja na changamoto zote za hali ya hewa na kilichotufanya tujitume ni umuhimu wa shughuli hii na kumbukumbu yake, katika historia ya nchi yetu.”

Awali kabla hawajaondoka vijana hao, waliagwa na Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, katika lango la Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro, huku akiwataka Watanzania kuwa na mazoea ya kujivunia Utanzania wao na kusema ujumbe ulioletwa na Kampeni hii ya Kilimanjaro, ulikuwa na maana kubwa kwa Watanzania.

Kampeni hii ilizinduliwa Julai 5, mwaka huu kwa lengo la kusherekea miaka 50 ya Uhuru na kuwakumbusha Watanzania kujivnia mafanikio, yaliyopatikana hadi sasa.

No comments:

Post a Comment