30 November 2011

Mafisadi CCM kung'oka rasmi

*Kamati ya Maadili sasa yapewa meno
*Mukama asema hakuna kurudi nyuma
*Viongozi waagizwa kuwachukulia hatua


Na Rehema Mohamed

CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza rasmi hatua ya kuwashughulikia watuhumiwa wa ufisadi ndani ya chama hicho kwa
kuiongezea nguvu Kamati ya Maadili kuwa Tume kamili yenye maamuzi.

Pia chama hicho kimeongeza idadi ya wajumbe wawili katika kamati hiyo na kuwaagiza viongozi wake katika ngazi zote, kuanza kutekeleza azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) iliyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma kwa kuwachukulia hatua haraka bila kupoteza muda watuhumiwa hao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho Bw. Wilson Mukama, alisema uamuzi wa kamati hiyo kuongezewa nguvu, unatokana na msimamo wa watuhumiwa kukataa kujiondoa wenyewe.

Alisema kutokana na hali hiyo, CCM inalazimima kuchukua hatua madhubuti ya kuwashughulikia watuhumiwa hao ili kuhakikisha maamuzi ya NEC, yanatekelezwa na kuweka wazi kuwa, chama hicho hakitarudi nyuma katika suala hilo.

“Mwenyekiti wetu (Rais Jakaya Kikwete), ametuomba tuzidi kulitolea ufafanuzi suala la maadili ndani ya chama chetu, viongozi wanaotuhumiwa, watafakari, wajitazame kisha wachukue hatua wao wenyewe;

“Katika kufanikisha hili, tumeamua kuiongezea nguvu na mamlaka Kamati ya Maadili kwa kuibadilisha kuwa Tume kamili bila kusubiri Kamati Kuu na kuongezea wajumbe toka 12 hadi 14,' alisema Bw. Mukama.

Alisema suala la maadili ndani ya chama hicho litaendelea kutiliwa mkazo kwani CCM ndiyo imeunda na maamuzi yake ni makini.

Aliongeza kuwa, chama hicho kimewaagiza watendaji wake katika ngazi zote kuanzia Taifa, Kamati za Siasa ngazi zote na Kamati ya Usalama na Maadili, kuanza mara moja mchakato wa kutekeleza azimio la NEC dhidi ya viongozi wanaohutumiwa kwa ufisadi ndani ya chama hicho.

“Hadi sasa takribani miezi saba imepita tangu azimio hili kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi zote ambao ni walengwa wa azimio hili,” alisema Bw. Mukama akimaanisha wale wanaotuhumiwa.

Aliongeza kuwa, “Bila shaka wakati umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio lake kuwawajibisha wahusika kwa kufuata utaratibu uliowekwa na kanuni za CCM za uongozi na maadili,” alisema.

Alitaja sehemu ya pili ya hatua hiyo kuwa ni kuwaondoa viongozi wanaotuhumiwa kwa nguvu chini ya utaratibu wa chama hicho ambao awali walipewa nafasi ya kutafakari, kujipima na kuchukua hatua wao wenyewe kwa maslahi ya chama.

Alisema kama wameshindwa kufanya hivyo, CCM italazimika kuwawajibisha na kusisitiza kuwa, hatua hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa haraka bila kuchelewa.

Katika hali inayoonesha kukasirishwa na kauli iliyotolewa na baadhi ya wana-CCM kuwa suala la kuwavua gamba viongozi watuhumiwa wa ufisadi limepita na kutamba wameshinda, Bw. Mukama alisema kama kuna mtu anadhani ameshinda si kweli bali hiyo ni hulka yake.

“Kama kuna mtu atatuhumiwa taratibu zitafuatwa dhidi yake, kama kuna mtu anasema ameshinda baada ya kikao cha hivi karibuni hiyo ni hulka yake, tume bado hatumhukumu mtu,” alisema.

Alisema CCM imefikia hatua hiyo kutokana na mwitikio mdogo wa azimio lilipotolewa katika mkutano wa NEC uliofanyika mjini Dodoma, Aprili 10 hadi 11 mwaka huu.

Akifafanua zaidi Bw. Mukama alisema, mtu akituhumiwa hatua ya pili inayofuata ni kufanyiwa uchunguzi wa juu ya tuhuma husika kwa kuhojiwa na taarifa kuwasilishwa katika kamati ndogo chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM na baadaye Kamati ya Usalama na Maadili itamalizia.

Bw. Mukamba alipotakiwa kutaja majina ya wanatuhumiwa alidai kuwa hadi sasa hawajapata mtu aliyetuhumiwa, akipatikana taratibu za uchunguzi zitafuatwa.

Katika kikao cha NEC, baadhi ya wajumbe walilalamika kuchafuliwa na kuhoji sababu za wanaowachafua kutochukuliwa hatua.

15 comments:

  1. WANANGUVU HIYO KWELI? YETU MACHO.

    ReplyDelete
  2. HUU NI UHUNI WA CCM. KUTANGULIZA UONGO NA UKWELI KWAO MWIKO DAIMA. JOPO LA WACHAWI WAKIKUTANA MATOKEO YOA NDIO HAYA, NA CCM HAWANA TOFAUTI NA WACHAWI.

    ReplyDelete
  3. tunaitaji vitendo wala sio polojo tu. ccm mna wadanganya wananchi.

    ReplyDelete
  4. Kikwete ameshindwa kukiongoza Chama Tawala.Hakuna maamuzi wazi yanayotoka kwake.Hawezi hata kuwataja kwa majina "WATUHUMIWA" kwa vile wengi ni marafiki zake wa karibu sana.
    Kwa hiyo,CCM imeachiwa iongonzwe na watu wasiokuwa na upeo wa kisiasa.Wengi wao hawawezi hata kufafanua maana ya demokratia kiupana wake. Wanakiongoza Chama kama wanavyoongoza familia zao nyumbani kwao. Hali hii ni hatari kwa Taifa letu.

    ReplyDelete
  5. Kweli inachekesha sana,Mukama anaulizwa awataje hao mafisadi watakaochukuliwa hatua na kujibu ya kuwa hakuna mtu ambaye ameshatuhumiwa mpaka sasa.Hii ndio aina ya viongozi ambao tunao,kwani hawajui na hawana uhakika hata wanacho ongea.

    ReplyDelete
  6. Mukama acha usanii, kama unasema hakuna mtu ambaye ameshatuhuma mara unasema hatua zichukuliwe kwa watu walioshindwa kujiondoa wenyewe, mara kamati imeongezewa nguvu zaidi ya wajumbe wawili, sasa imeongezewa nguvu kupambana na nani iwapo unadai hakuna mtuhumiwa? kama maelezo yako yanamegeka namna hiyo je utakuwa na ujasiri wa kupambana na mafisaidi kweli mmh.

    ReplyDelete
  7. Michezo ya kisiasa

    ReplyDelete
  8. Mukama si muwazi,kuufisha ukweli juu ya ufisadi unaofanyika ndani ya nchi hii na baadhi ya vigogo wa CCM utaingamiza ccm na nchi yetu,tukimbilie wapi? Mukama be serious kusimamia azma ya CCM kujivua gamba.porojoporoja zako za kila siku zimetuchosha.

    ReplyDelete
  9. Musiwe na haraka, mambo karibu yataiva tu, tusiwe napapara

    ReplyDelete
  10. Ebu fanyeni kweli CCM, hata sisi ambao hatumo ktk siasa tuone kuwa usanii mmeuwacha.
    Papa na manyangumi yoote yanafahamika mnawaogopea nini ? hao si malaika wala manabii.
    Jengeni heshma ya Chama chenu.

    bwerekasumba.

    ReplyDelete
  11. siasa za maji taka ndio kama hizo,kulindana,kufichana,kuogopana, yote hayo faida za kukosa maadili na uadilifu,bado tutasikia mengi.

    ReplyDelete
  12. kweli kaka, ABRAKADABRA naiona live.

    ReplyDelete
  13. Hakuna kitu, Mwenyekiti mwenyewe hayuko sirious bana. Anatushia nyau watu wazima. Mbona miezi mitatu imeisha lowasa na chenge wapo na hawezi kuwafanya kitu.

    ReplyDelete