16 December 2011

Posho zamkera Polycarp Pengo

*Asema Watanzania wataichukia nchini yao, serikali
*Asisitiza kushuka ufaulu kunatokana na elimu duni
*Awataka wananchi kuacha mzaha suala la katiba
*Apongeza uamuzi wa serikali kukataa ushoga


Na Peter Mwenda

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amesema kitendo cha wabunge kuongezewa posho, kitawafanya
Watanzania kuichukia nchi yao, viongozi na serikali iliyopo madarakani.

Kardinali Pengo aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari habari wakati akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi na Mwaka Mpya na kuhoji kuwa, kama mbunge anapata mshahara mkubwa, kwanini aongezewe posho wakati taifa linahitaji fedha ili kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Alisema ili taifa lipate maendeleo ya kweli, asiwepo kiongozi yeyote anayetumia nafasi yake kujilimbikizia posho badala ya kufanya kazi kwa bidii na kufikiria jinsi ya kuboresha maisha ya Watanzania ili waondokane na umaskini walionao.

Alisema Serikali ya Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, aliamini kuwa ili taifa lipate maendeleo ya kweli, lazima Watanzania wafanyekazi kwa bidii ili kufikia malengo waliyonayo.

Aliongeza kuwa, ajali za barabarani zinazotokea kila siku hazina maana kuwa Tanzania kuna magari mengi kuliko mataifa nyingine bali ni ishara ya ukosefu wa maadili mema.

“Ajali zinasababisha vifo vya watembea kwa miguu, ni wazi kuwa Watanzania wamekosa maadili yanayoweza kurekebishwa, wananchi wanapaswa kubadilika na kukubali kuwa kila kitu kisicho na faida hakipaswi kupewa nafasi,” alisema Kardinali Pengo.

Akizungumzia Katiba Mpya, alisema ni vyema Watanzania wajue kuwa, mchakato wake si jambo la kufanyia mzaha.

“Novemba 30 mwaka huu, nililetewa barua iliyonitaka nitoe maoni yangu kuhusu katiba na kuyawasilisha Desemba 4 mwaka huu, bahati mbaya siku hiyo nilikuwa safari lakini bado niliomba nitoe mawazo yangu kwa maandishi.

“Kimsingi utaratibu huu si sawa, siku nne hazitoshi kumfanya mtu kutoa mawazo yake kuhusu jambo kubwa kama hili, yawezekana watu wanaohusika na jambo hili hawako makini,” alisema.

Alisema Rais Jakaya Kikwete amebakiza miaka minne ya kuiongoza Tanzania hivyo amewataka Watanzania wajue kuwa, rais ajaye atatokana na matakwa ya Katiba Mpya si vinginevyo.

Kardinali Pengo alisema, kama Watanzania watashindwa kutoa maoni yao kikamilifu, mawazo yao hayataingizwa katika katiba kwani nchi nyingi barani Afrika na Duniani, zimejikuta zikimwaga damu kwa sababu ya Katiba.

Akizungumzia ushoga, Kardinali Pengo aliipongeza serikali ya Tanzania kupinga vikali shinikizo la kuruhusu vitendo hivyo.

“Inashangaza kuona baadhi ya viongozi katika mataifa mengine wanashawishi serikali yetu itekeleza mambo ambayo ni kinyume na utamaduni tulionao, huu ni wendawazimu, ni bora tuendelee kuwa maskini kuliko kutegemea misaada yenye masharti,” alisema.

Akijibu maswali ya waandishi kuhusu maendeleo ya elimu nchini, Kardinali Pengo alisema kushuka kwa kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi, kunatokana na elimu duni inayotolewa na serikali kushindwa kuwa wazi.

“Wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanatakiwa kujua namna ya kudai haki kwa njia ya demokrasia badala ya kulazimisha kile wanachotaka kwa sababu kesho na kesho kutwa, wao ndiyo watakuwa viongozi,” alisema.

Alisema matukio ya kuandamana, kuvunja nyumba, kuzuia magari yasipite barabarani na kufikia hatua ya kutumia silaha si njia ya kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.

Aliongeza kuwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELSB), haipaswi kubagua mikopo wanayotoa kwa kuangalia watoto wa vigogo na kuwaacha watoto wa wakulima.

Akizungumzia mfumo wa vyama vingi vingi vya siasa nchini, alisema Tanzania haijawa tayari kuwa na vyama vingi kwani kuna kila dalili kuwa, mawazo ya chama kimoja ndio yanayopewa nafasi.

7 comments:

  1. Chadema mnaambiwa na Kadinali hayo ingawaje kaelekeza kwa wanafunzi wa chuo kikuu lakini ni mfano mzuri kwenu pia,leo mnalazimisha mambo kwa nguvu la sivyo damu itamwagika lakini kesho mkiongoza nchi mkiwapa amri wananchi wakikataa ndio damu itamwagika? Hongera Kadinali wape mafunzo ya busara,hata huko chuoni hiyo migomo ina mikono ya watu wasio na busara ambao wanazorotesha elimu kwa makusudi kabisa.

    ReplyDelete
  2. maaskofu acheni kujiingiza kwenye siasa , chagueni moja, wito kwa serikali kupuuza viongozi wote wa dini wenye kukemea serikali au kusifu , inatakiwa serikali isiwe na dini wala kuelemea upande mmoja, wito kwa vyombo vya habair kuacha kutangaza maneno ya maaskofu au viongozi wowote wa kidini, mnaipeleka nchi kubaya

    ReplyDelete
  3. Jamani watanzania wenzangu kuna sababu gani za msingi za kutoona ukweli wa Baba Pengo? Mimi nadhani inatubidi kumpongeza siyo kuwa vipofu kiasi hicho. Yote aliyosema hata mwanangu wa chekechea anasema kila siku tunapokuwa mezani. ni ajabu wewe mtu mzima huoni ukweli huo. Tumpongeze askofu Pengo kwa kauli hiyo ya uwazi. Mafisadi mkiguswa mnaanza kusema Udini? Acheni unafiki? Uongozi wetu mbovu ndiyo maana tuna matatizo mengi tena ya msingi. Hongera baba Pengo, tuonyeshe mapengo yote ya serili tupo nyuma yako. Katika msikiti wetu hakuna mtu anayeongea uozo wa serikali kwani tumepata mgao juzi tu wa zawadi ya Xmas. Kaeni chonjo

    ReplyDelete
  4. ikiwa mtoto wako wa chekechea anaweza kujua na kuzungumzia hayo basi hio ni ushahidi kamili kuwa askofu kachemsha kazungumza mambo yanayojulikana hata na watoto, aingie kwenye ulingo wa siasa aache dini , hatutaki ktk serikali yetu udini wa aina yoyote, vyombo vya habari vipigwe marufuku kuandika habari za udini, serikali yetu haina dini kikatiba ( sijui kama ni kweli au tumefungwa kamba kama mbuzi )

    ReplyDelete
  5. Katiba mpya ndilo litakuwa jiwe la shingoni kwa nchi yetu. Namna mpangilio wa mambo unavyokwenda sasa hivi, ni Chama tawala na serikali yake ndio watakaotutengenezea katiba. Sina uhakika kama wananchi watakubaliana na matokeo ya kazi hiyo wakati watakapotakiwa kupiga kura ya maoni kuipitisha au kuikataa. Kama watakuwa wameandaliwa vyema na kupata uelewa wa kutosha, ninaamini hawatakubaliana na udanganyifu huu unaoendelezwa na Kikwete na washirika wake.

    ReplyDelete
  6. Sio jambo baya kama kiongozi wa kidini akikemea maovu yanayotokea katika nchi yetu. Anao uhuru wa kujieleza kama raia na kutoa dukuduku lake kama analo. Lakini pia tukumbuke kuwa kama nchi isingekuwa na ubadhirifu askofu asinge sema lolote. Maana watu anaowaongoza wanateseka na hii kazi kapewa na mungu. kama hatakemea siku moja ataulizwa na mungu siku ya mwisho.Je hukumbuki jinsi Musa alivyowaongoza wana wa Islael toka jangwani Misiri?

    ReplyDelete
  7. Jamani askofu,shekhe na wachungaji ni raia halali wa nchi hii,ni hatari zaidi kama taifa linaelekea kubaya huku viongozi wa dini wakikaa kimya pasipo kukemea ubaya huo,ninavyofahamu ni hatari kama viongozi wa dini wakitumiwa na mtu yeyote yule kwa masilahi yake binafsi ikiwemo kumsafisha kisiasa au kupigia debe chama fulani cha siasa,kwa hiyo tusikimbilie kuwashutumu pale wanapotoa angalizo sahihi,au ushauri juu ya jambo la msingi kwa jamii au taifa letu,tuwape nafasi ya kuikosoa jamii yao wanayoishi ambayo nao ni sehemu ya jamii hiyo.

    ReplyDelete