29 December 2011

Polisi kizimbani kwa kudhalilisha watoto 3

Rehema Mohamed na Paulina Lyapa

POLISI mwenye namba D 5882 Koplo Richard Singano (47) wa Kituo Kidogo cha Gongo la Mboto amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa
tuhuma za kuwadhalilisha kijinsia watoto watatu.

Akisomewa shtaka hilo mahakamani hapo jana na wakili wa serikali, Bi.Elizabert Kaganda, alidai watoto hao wana umri wa miaka saba, nane na tisa na kwamba mtuhumiwa alitenda kosa hilo Desemba 21, mwaka huu maeneo ya Kituo cha Polisi Gongolamboto.

Mbele ya Hakimu Bw.Lead Chamshama, Bi.Kaganda aliiambia mahakama hiyo kuwa mtuhumiwa huyo alifanya kosa kwa kuingiza vidole vyake sehemu za siri za watoto hao kwa nyakati tofauti huku akijifurahisha kitendo ambacho ni kosa la jinai.

Mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo. Upande wa Jamhuri uliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuomba tarehe kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Chamshama, alipanga Januari 17, mwakani kuwa ni siku ya mshtakiwa kusomewa mashtaka. Mshtakiwa alirudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana.

Mahakama hiyo ilimtaka mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya sh.milioni moja na mmoja kati yao awe mfanyakazi wa serikali au taasisi inayotambulika kisheria.

Katika hatua nyingine mfanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw.Patrick Hegen (30), amepandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa tuhuma ya kuunganisha nishati hiyo bila idhini ya mwajiri wake.

Mbele ya Hakimu, Bw.Genivatus Dudu, wakili wa serikali Bw. Charles Anindo, alidai mahakamani hapo kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo kati ya Mei sita na Juni 30, mwaka huu eneo la Mbagala Vigozi Manispaa ya Temeke.

Ilidaiwa kuwa mtuhumiwa huyo aliingiza umeme katika nyumba ya Bw.Jamal Sudi na kuisababishia TANESCO hasara ya sh.milioni 3,600,000.

Mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo na kurudishwa rumande baada ya kushindwa masharti ya dhamana ambavyo ni kujidhamini mwenyewe kwa kuwasilisha mahakamani hapo fedha taslimu sh.milioni tatu kusaini bondi ya sh.600,000.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 10 mwakani.

No comments:

Post a Comment