29 December 2011

Kamati kumjadili Hamad Rashid Des. 30

*Tuhuma zake kufikishwa Baraza Kuu kwa uamuzi

Rehema Maigala na Surah Mushi

SIKU moja baada ya Mbunge wa Wawi, Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Bw. Hamad Rashid Mohammed kukataa kuhojiwa na Kamati ya Nidhamu na
Maadili ya chama hicho, tuhuma zinazomkabili mbunge huyo zitafikishwa kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji Taifa.

Kikao hicho kinatarajia kukaa Desemba 30-31 mwaka huu na baadae kupelekwa Baraza Kuu kwa maamuzi zaidi.

Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Ofisa Matukio wa chama hicho Bw. Abdulrahman Lugone, alisema suala la Bw. Mohammed litazungumzwa katika vikao hivyo kwa kuzingatia mwongozo wa katiba ya chama hicho.

Alisema hivi sasa chama hicho kimeanza mahojiano na wajumbe wa Kamati ya Maadili, baadhi ya viongozi wa chama na wanachama mbalimbali juu ya uamuzi wa Bw. Mohammed, kukataa kuhojiwa na kamati hiyo.

“Kwa sasa hatuwezi kusema lolote, tunasubiri vikao ambavyo vitakaa na kufanya uamuzi kwa kuzingatia mwongozo wa katiba ya chama chetu.

“Inawezekana Bw. Mohammed hana kosa lolote hivyo kama leo hii tutasema lolote kabla ya vikao, tutakuwa tumemuhukumu bila sababu, naomba muwe na subira,” alisema Bw. Lugone.

Juzi Bw. Mohammed alikataa kuhojiwa na kamati hiyo kwa madai kuwa baadhi ya wajumbe wake, hawana sifa zinazostahili.

Alisema utaratibu uliotumika kuwateua wajumbe hao, haukuzingatia kanuni na taratibu hivyo hakuwa tayari kuhojiwa na kamati hiyo.

''Mimi binafsi sina tatizo na suala langu kupelekwa kwenye Kikao cha Baraza Kuu, nipo tayari kwenda kuhojiwa nikiitwa ili niweze kujibu tuhuma za kukiuka utaratibu na katiba ya chama,” alisema Bw. Mohammed wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Aliongeza kuwa, migongano inayoendelea ndani ya chama inatokana na majungu yaliyokithiri ndani ya chama hivyo ni wazi kwamba hakifanyi kazi kama taasisi.

No comments:

Post a Comment