28 December 2011

Polisi Iringa 'yaota' kucheza Mapinduzi Cup

Na Zahoro Mlanzi

TIMU ya Polisi ya Iringa, imepanga kukaa meza moja na waandaji wa mashindano ya Kombe la Mpinduzi, kuomba wapewe nafasi ya mabingwa wa soka Tanzania Bara, Yanga ambayo
inasuasua kuthibitisha kushiriki mashindano hayo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa timu hiyo, Abdul Changawa alisema baada ya kusikia timu ya Yanga ikisuasua kuthibitisha, wameona sio mbaya kama na wao wakishiriki sherehe hizo za Mapinduzi kwa kuwepo katika mashindano hayo.

Alisema jana mchana alitarajiwa kwenda viziwani humo kuonana na waratibu kuzungumzia hilo kwani ana amini hakuna linaloshindikana na kubwa zaidi wamejiandaa vizuri.

“Tunasikia kocha wao (Yanga), Kostadin Papic amefuta mechi zote za kirafiki na kombe hilo, hivyo kwakuwa sisi tumeshajipanga kimchezo, tunakwenda kuonana na wahusika watupe sisi hiyo nafasi,” alisema Changawa.

Akijibu swali kuhusu kanuni za mashindano hayo ambayo kwa upande wa Bara zinatakiwa timu zilizoshika tatu bora katika Ligi Kuu, alisema kwakuwa muda ni mfupi, halitakuwa jambo rahisi kupata timu lakini wao wameshajiandaa kwa hali yoyote.

“Unajua mashindano yale yana gharama zake, lakini sisi tukishiriki sidhani kama tutakuwa sehemu ya gharama hiyo na pia kama itashindikana basi ila lengo letu ni kusherehekea pamoja na wenzetu wa visiwani,” alisema Changawa.

Pia alizungumzia maandalizi ya timu katika ushiriki wa Ligi Daraja la Kwanza itakayoanza Januari 20, mwakani, alisema wana mpango wa kupiga kambi Dar es Salaam ili kujiandaa na ligi hiyo.

Alisema katika ligi hiyo timu yao ipo nafasi ya pili katika kundi lao na tayari kambi imeshaanza na mambo yakienda vizuri watakuja Dar es Salaam kwani kikubwa kilichowakwamisha ni mafuriko.

No comments:

Post a Comment